Saturday, January 13, 2007

AFRICA


Afrika inavyodharaulika na wazungu

Na Nyasigo Kornel


Afisa mmoja wa Marekani aliyekuwa akisimamia misaada inayolewa na nchi hiyo kwa nchi za Afrika aliwahi kuongea kwa majigambo akisema kuwa ‘Principle export of the United States to Africa is money (bidhaa kubwa anayoisafirisha Marekani kuja Afrika ni pesa)’.

Kuna kikundi cha wazungu wanaofikiri kuwa Afrika ikinyimwa misaada na nchi tajiri inaweza ikapukutika na kupotea katika ramani ya viumbe hai wa dunia hii.

Katika kitabu chake Jacob Akol kiitwacho Burden of Nationality (Mzingo wa Uzalendo) aliwajibu wazungu hawa wanaoidharau Afrika akiwaambia kuwa Afrika itaendelea kuwepo hata ikifungwa milango yote ya misaada kwa maana misaada hiyo anayoiimanisha haimwinui mwafrika kwa lolote bali na kumdhalilisha na umjengea akili tegezi.

Historia ya biashara ya utumwa, ukoloni na misaada wanayotupatia wazungu imekuwa ikipumbaza viongozi wetu na kuwafanya vibaraka wa wazungu, makampuni yao na sera zao. Na zaidi zimemfanya mtu mweusi apoteze dira na kujidharau mbele ya mzungu.

Moja ya kikundi kilichojikita katika kulichukia sana watu weusi kiitwacho ‘anti-blacks’ huko Ulaya Magharibi hasa katika nchi za Italia, Hispania, Ujerumani na baadhi kutoka Uingereza na Marekani walikuwa wakijiuliza maswali kwenye vyombo vya Habari kuwa “Kwani Afrika ni nini kwetu mpaka tuisaidie? Kwa nini Afrika isiachwe ife na ikapotea katika ramani?”

Wazungu hawa nao walikuwa na hoja, walikuwa wakisema kuwa Afrika ina mali asili nyingi sana na wasomi sasa walikuwa wameongezeka kwa kiasi kikubwa, lakini ilikuwa haiwezi kuzalisha hata chakula chake.

Katika gazeti la Marekani iitwayo Time-Warner ilidiriki kuandika kuwa chakula kinachozalishwa katika ukanda wa mahindi wa kule Marekani ni kubwa kuliko mahindi inayozalishwa Afrika nzima na visiwa vyake. Na hivyo aliwahi kuishauri Marekani kutoa chakula cha ng’ombe ili igawanywe katika nchi zenye njaa barani Afrika.

Mwingine aitwaye Jamie Glazov katika kitabu chake aliyoiandika ya White Guilt alisema kuwa Afrika ikiendelea kuishi itachangia kuenena kwa kasi kwa magonjwa yanayotibika na hasa katika nchi za tropiki, kwa sababu serikali zao haziwezi kudhibiti hata ugonjwa unaotibiwa kwa senti moja ya Marekani.

Katika gazeti la Serikali la Ufaransa liitwalo Le Monde mwandishi wake mwenye asili ya Poland aitwaye Krzysztof Crosstie aliandika makala ikiuliza juu ya uwezo wa kufikiri wa Mwafrika na akaendelea kuuliza kama kweli Mungu alimuumba mzazi mmoja Adam na Eva. Alikataa na akasema kuwa anaamini katika mabadiliko ya maumbile kama anavyoeleza Charles Darwin katika nadharia yake ya mabadiliko katika maendelao ya binadamu.

Kuna baadhi ya machapisho ambayo yamekuwa yakitolewa na wazungu kukejeli Uafrika kila mara na kuonyesha kuwa Uafrika ni nusu ya maumbile na kuwa ndiye kiumbe aliyekaribu na nyani katika mtiririko wa maumbile.

Baadhi ya machapisho hayo ni kama vile The Missing Link, Racial Blasphemies, Black Rood, Ambiguous Identity, The Black Batch, A Thief In Babylon, White Guilt, Is your Father Black na Black Lies- White Lies. .

Kumekuwepo hata na midahalo ya kujadiliana iliyoendeshwa na gazeti la Readers Digest juu ya bara ipi yenye watu wenye uwezo wa juu wa kufikiri, mara nyingi Afrika anakokaa mtu mweusi imekuwa ikiwekwa ya mwisho katika fikra.

Ubabe huu wa kutaka kuingiza katika akili zetu kuwa sisi ni wajinga na watu dhaifu na wa chini hauishii hapo tu.

Michael Paul Rogin anaandika katika kitabu chake kiitwacho Black Face, White noise akisema kuwa waandaaji wa picha za sinema wa Holywood ambao wengi walikuwa ni Wamarekani wenye asili ya Kiyahudi walikuwa wakimdharau Mwafrika na hata kumwonyesha kama kiumbe dhaifu asiyestahili kiakili na hata kutendewa haki.

Baadhi ya sinema zinazomwonyesha mtu mweusi kama kiumbe kisichofaa ni kama vile ‘Gone with the Wind, Pinky, Home of Brave, Intruder in the Dust, The Jazz Singer and Whoopee’.

Na hata hivyo picha nyingi za high-tech utawakuta wazungu wa Holywood wakichaguana wao kwa wao na akiwepo mtu mweusi anakuwa ni chambo au mtu wa kutafutwa na ule mtambo, ili mradi tu ionekane kuwa mtu mweusi ni dhaifu na kuwa mzungu ashindwi.

Ni mpaka muda wa hivi karibuni ndio mwandishi kama Osca aliyeandika sinema ‘Crash’ iliyochezwa na Robert Jensen alipopewa zawadi ya kwa kuandika sinema iliyotoa taswira nzuri ya mtu mweusi.

Siku sio nyingi nilikuwa nikisoma mahojiano ya moja wa mawaziri wa zamani wa Rais Kabila alipokwenda Marekani katika gazeti moja liitwalo The Economist, badala ya mwandishi yule kumuuliza Waziri huyu alichokifuata Marekani, aliuza kuwa msaada gani unaotegemea kuupata kutoka hapa Marekani!

Wamarekani wanaamini kuwa viongozi wetu wakienda kule kwao wamekwenda kuombaomba au kutafuta msaada.

Ndio maana tuna jukumu la kuwauliza viongozi wetu kama Afrika imechoka kiasi hicho cha kujulikana na kama ombaomba, je Afrika bila msaada hata ya shilingi moja ya wazungu itapotea katika ramani? Na hiyo misaada imefanya nini kutufutia aibu ya kudharauliwa?

Sio siku nyingi mchezaji wa Barcelona- Hispania anayetoka Afrika aitwaye Samwel Eto alikuwa akizomewa na wazungu na kuonyeshwa kuwa anafanana na nyani, je wazungu wanapata jeuri wapi kama sio sisi ndio tunawapa penyo hizo?

Siku moja katika miaka ya nyuma niliporudi likizo nyumbani kijijini kutoka chuoni hapa Dar es Salaam, mzee mmoja aliyestaafu kazi baada ya kufanya kazi kama Afisa Elimu wa Wilaya wakati wa Mwalimu Nyerere aliniuliza kama ninaweza kujuana na mzungu yeyote ili nimuunganishe naye aweze kumwandikia kwa maana alikuwa akipata shida ya kuwalipia watoto watano ada ya shule katika shule za binafsi.

Hata nilipojaribu kumkwepa maana sikupenda ampe mzungu mtazamo huu ambao umekuwa ukitudhalilisha sana, alizidi kuniuliza kila siku kuwa, “Wewe kijana umesoma shule za seminari, ulikuwa ukifundishwa na wazungu, huna rafiki hata mmoja unipe niwasiliane naye! Wewe kijana ulikuwa unachezea bahati!”

Sasa huyu mzee ni Afisa Elimu hana malengo ya namna ya kutumia sehemu yake ya akili iliyobaki kubuni miradi midogomidogo, muda wote katika maono yake anamwona tu mzungu kama mkombozi wake na wala sio fikara zake.

Kijana mmoja aliyekuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliwahi kupata anwani ya barua pepe ya mzungu na kuanza kuwasiliana naye kwenye, alichokifanya huyu kijana wa chuo kikuu ni kuanza kueleza shida alizokuwa akitaka msaada wa kipesa, kumbe hakujua kuwa aliyekuwa anawasiliana naye ni mtoto mdogo wa miaka sita alyekuwa akisoma hatua ya pili huku nchini kwao.

Wazazi wa yule mtoto walimwandikia huyu kijana wa chuo kikuu kulaani hatua hiyo ya kumwomba mtoto mdogo wa miaka sita pesa.

Wa tatu kama ni mchungaji wa kanisa moja changa linaloendesha kazi zake hapa mjini Dar es Salaam, amesajili kanisa lake linalohubiri wokovu. Siku moja alilazimika kumsaidia mzungu kubeba mabegi ile mikubwa wakiwa wanatafuta tiketi ya yule mzungu aliyetaka kusafiri kwenda Mafia, walizunguka kwa masaa matatu.

Mwishoni baada ya usafiri wa siku ile kushindikana alimwomba yule mzungu kwenda kulala kwake, na baada ya pale waliachiana anwani na hivi karibuni alikuwa akitoa ushuhuda jinsi Mungu alivyomsaidia kumkutanisha na mtu ambaye sasa alikubali kumtumia dola mia kila mwezi.

Mzungu yule alifikiri kuwa mchungaji yule alikuwa akifanya wema kama mchungaji, kumbe wema anaouonyesha Mwafrika huyu dhaifu kwa mzungu ni kuwekeza.

Huu udhaifu auhishii hapo, nilipokuwa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, wazungu walikuwa wakija kwa awamu katika kozi fupi na nyingi zilikuwa ni masomo ya ‘arts’.

Vijana wengi walilazimika kujenga nao uhusiano hata kama haukuwatoka rohoni, walijitahidi kulazimisha kuongea kiingereza kwa matamshi yale ya kizungu ili mzungu ajisikie kuwa yeye hana utofauti na vijana wa kizungu.

Kwa kijana wa Kiafrika, na hasa walio wengi, na zaidi wasio na mwamko wa kifikira, wanaona kabisa kuwa kule kusalimiana na mzungu ni bahati na kulala naye kimapenzi ni suala la kutangaza na linaweza kumtenga hata na jamii yake kubwa ya Waafrika.

Katika masimulizi ya safari za James Bandrick alipotembelea mji wa Buhemba-Mara katika kipindi kile dhahabu zilipokuwa zikikusanywa na hao wazungu kupeleka kwao, mmoja ya familia kutoka katika jamii ya Wanata aliyoifikia, baba wa ile familia alilazimika kumwachia kitanda chake huyu mzungu na kisha yeye kulala chini kwenye ngozi sakafuni na mke wake.

Safari yake ilichukua wiki mbili, aliwasifu Waafrika kwa ukarimu, na alifikiri alikuwa amewajua Waafrika walivyo, siku ya mwisho alipokuwa anaondoka, aliangalia kwenye sanduku hakuona viatu, baadhi ya pesa, nguo na hata vitu vingine vya thamani vilikuwa vimeibwa.

Mwishoni alikiri kuwa ni vigumu kumfahamu Mwafrika kwa siku moja, kwa maana wema wao hauwatoki rohoni, kwetu wema ni tendo la mazoea na mila wala haionyeshi undani wa Mwafrika. Kwani hata unaweza kukaribishwa kula chakula kama tendo la mazoea na ukisha kula na kuondoka wakakusema.

Mama mmoja wa Kitanzania alikuwa ameolewa na Mjerumani na alikuwa akiishi naye mjini Dar es Salaam, siku ilipofika ya kwenda kujua kwao huyu dada kijijini, ilimlazimu huyu dada kumpeleka Mwanza kwa kaka yake.

Alipoulizwa na wazazi wake sababu ya kumpeleka mkwe mzungu kwa kaka yake badala ya nyumbani kwao ili nao wakapate ufahari kuwa binti yao ameolewa na mzungu, yule binti aliwaambia kuwa mme wake angeona ajabu kunya kwenye choo cha nje, tena choo cha shimo!

Ukipita mitaa ya Samora, Posta Mpya au Posta ya Zamani mjini Dar es Salaam, ni mitaa iliyo na wazungu sana, hasa wale wanaotaka kusafiri kwenda Zanzibar au kufanya ununuzi, kupata vibali mbalimbali za kuingia nchi nyingine, utaona vijana wakitanzania wakiwa wamejipanga wakiwakimbilia hawa wazungu na hata wale wasiojua kiingereza hujitahidi kwa namna yake ili mradi apate urafiki, amsindikize anakokwenda na hatimaye mkono uende kinywani.

Mwalimu wangu mzungu aliyenifundisha nikiwa katika kidato cha kwanza aliwahi kuniandikia baruapepe hivi majuzi katika barua hiyo moja ya vitu alivyoniambia ni kuwa kama kuna msaada wowote wa kipesa anaoweza kunipa katika shughuli ninayofanya nimjulishe.

Hivi sisi Waafrika hatuwezi kufanya mambo yetu mpaka msaada, hivi wazungu wanatupa mtazamo gani na wanatungalia kwa jicho gani? Ni lini tutawaonyesha kwa vitendo kuwa tunajiamini, tunaweza bila wao na kwamba wao sio Miungu watu walioletwa kuikomboa Afrika.

Wiki mbili kabla ya siku ya mtoto wa Afrika, nilifanikiwa kuhudhuria Zanzibar ilipokuwa ikifanyika kwenye moja ya hoteli ambapo tulikusanyika vijana wapatao 25 wa Kiafrika na wazungu idadi yao ilikuwa 20. Kama unavyojua Waafrika tunavyopenda kujitenga na kukaa peke yetu tukijadili mambo yetu.

Wahudumu wa ile hoteli wote waliwakimbilia wale wazungu na hata sisi kupata huduma nusu saa baadaye, wenzetu waliotoka Afrika ya Magharibi walianza kufoka na kufanya fujo wakisema sehemu zingine za bara hili Afrika bado inatawaliwa na wazungu!

Tunasikia katika masimulizi za Mabutu Seseseko kuwa maji yake ya kunywa yalikuwa yakitoka Ufaransa kwa ndege wakati mto Kongo ukisifika duniani kwa kuwa mto mkubwa na wenye maji masafi sana.

Charles Jonjo wa Kenya naye kuna kipindi tunaambiwa kuwa alikuwa akila vyakula vya makopo tu kutoka Ulaya na kwamba akidharau vyakula vya Kenya pamoja na kwamba vyakula vya asili ni vizuri kuliko vya makopo!

Dumnont katika kitabu chake cha Afrika Inakwenda Kombo aliwahi kutembela Afisa mmoja katika serikali ya Guinea Bissau, yule Afisa alipomwona kuwa ni mzungu alimletea juisi ya maembe ya makopo, Dumnont alikataa akamwomba kama ana maembe ya kawaida ampe au la, amtume mtu sokoni akamnunulie.

Yule Afisa alikataa kuwa sokoni hakuna maembe, kitabu kinaelezea kuwa alipokwenda mwenyewe sokoni alikuta maembe mengi na mengine yamekosa wanunuzi.

Na hivyo ndivyo hata ndugu zetu wengi Watanzania, wako tayari kununua maboga yaliyoletwa kutoka Afrika ya Kusini kwenye masoko kama shoprite, kuliko kunua maboga ya Kariakoo. Yuko tayari kununua mvinyo kutoka Italia na kuacha Tanganyika Wine ambayo ingemgharimu kiasi kidogo sana.

Siku ya maonyesho ya sabasaba Afisa Biashara mmoja aliyekuwa akisimamia banda lililokuwa na majani fulani yaliyotumika kutengeneza juisi, alikuwa akisisitiza kutumia vyakula vya asili na sio vya dukani, tulipowatembelea ofisini kwao kwa mahojiano zaidi baada ya maonyesho walitukaribisha kwa kutupatia juisi za Afrika ya Kusini iliyosindikwa kwenye makopo na sio juisi ile ya kwao inayotokana na majani ya mmea wa asili.

Dhana hii haijawatoka wengi, sio wasomi, wenye pesa, wanafunzi, wakulima, waliosoma Ulaya na hata viongozi wakubwa wa nchi zetu.

Dr. Martin Luther King Jr aliyepigania haki za watu weusi aliwahi kusema kuwa maisha ya mtu yanafikia kikomo siku ile anapoanza kukaa kimya juu ya mambo ya msingi yanahusu maisha yake.


0715 551455


No comments: