Saturday, January 13, 2007

WASOMI


Wasomi msitumike kupotosha umma

Na Nyasigo Kornel


Ukitaka kuona genge wasomi waliokosa dira kwa mwenendo na uchungu wa demokrasia katika nchi hii basi nenda katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) utapata kikundi kimoja cha hao wasomi wakiwa wameanzisha asasi iitwayo REDET, asasi ambayo imekuwa ikitumika kuhujumu fikira za wananchi kwa kutoa takwimu zenye maoni zinazoonyesha kuwa hii ni asasi ya Rais Jakaya Kikwete.

Watu wanategemea Chuo kikuu kiweze kuwa chachu ya kuelemisha jamii, kufanya tafiti zinazosaidia katika kuboresha na kutoa changamoto kwa raia, lakini kinachofanywa na REDET ni tofauti kabisa.

Mwaka jana katika mchakato wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2005, REDET ilikuja na tafiti zilizokuwa na lengo la kumjengea jina Rais Jakaya Kikwete, wakati huo alikuwa mmoja wa wagombea katika kinyanganyiro hicho cha kumtafuta Rais wa nchi.

Katika tafiti hizo REDET ilikuwa ikiweka idadi kubwa ikiwa inaonyesha kuwa Kikwete ndio chaguo la watu na wagombea wengine walikuwa wakipendwa kidogo tu na watanzania.

Kama kwamba hiyo haikutosha, na hata baada ya Rais Kikwete kupata Urais tulitegemea wangeendelea na tafiti zenye maana katika kuamsha hari ya siasa nchini, lakini wanaonekana kuwa bado ni kikundi cha kueneza propaganda tu za kupumbaza watanzania.

Mwezi mmoja tu uliopita aliyekuwa Mkurugenzi wa REDET Prof. Rweikaza Mukandala alifanikiwa kuwa Makamu mkuu wa chuo Kikuu cha Dar es Salaam jambo ambalo wengi waliliona kama mkono wa Rais wa nchi katika kumshukuru kwa kulitumia REDET kumpa Rais mwonekano mzuri mbele ya jamii.

Rais Kikwete alipomaliza siku 100 ofisini, REDET iliyokuwa ikiongozwa na Prof. Rweikiza Mukandala ilikuja na takwimu kuwa umaarufu wa Rais umefikia asilimia 84 na kwamba bado wananchi wana matumaini naye makubwa na hasa pale serikali yake iliposaka wezi na majambazi kwa nguvu zote.

Watu walisema kuwa hizi ni nguvu za soda, na sasa wananchi walisubiri kuona kama masula ya msingi katika mstakabali wa kitaifa zinapewa kipaumbele kama suala la rushwa.

Mwezi uliopita vyombo vya Habari vimekuwa vikiiandama serikali ya awamu ya nne kwa kushindwa kushughulikia suala la umeme na kulifumbia macho suala la rushwa kwa viongozi ambao hata hawajamaliza mwaka tangu wapewe madarakani, wengine watoto wao wakiwa wameshirikishwa katika tuhuma za Richmond.

Ili kumsafishia jina Rais ambaye sasa umaarufu wake ule umeingia doa baada ya kutoa ahadi katika kila kona ya Tanzania zikiwa na mwonekano duni kutimia huku wakisingizia ukame na umeme, tayari REDET na wasomi wake walikusanya waandishi wa vyombo vya Habari mbalimbali tayari kwa kusafisha tena Rais Jina la Rais Kikwete kwa wananchi wake.

Kama haitoshi mwezi jana Rais Kikwete alipokuwa akiadhimisha mwaka mmoja tangu apewe madaraka, REDET hawakuwa na jipya bali na Makamu mwenyekiti wa REDET Dr. Laurian Ndumbaro kutoa ripoti yao kuwa umaarufu wa Rais umepungua kutoka asilimia 84 hadi asilimia 67.

Ili kuongeza chumvi zaidi ripoti ile ya hawa wasomi inamkwepesha Rais kwenye Serikali yake kana kwamba yeye na serikali ni vitu viwili tofauti, ikisema kuwa wananchi waliotoa maoni walionekana wakiridhika na kuwa na imani kwa Rais Kikwete kama mtu binafsi, huku walio wengi hawakuonyesha kuridhika na utendaji kazi wa taasisi za serikali.

Kwani wasomi hawa wanataka kutuambia kuwa Rais na serikali yake ni vitu viwili tofauti au wasomi hawa wanataka tuamini kuwa Rais anafanya kazi vizuri huku akiwasamehe watendaji kazi wabovu aliowateua yeye tuliyempatia kura zetu, sasa hapo nani ni mbovu?

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alichaguliwa ili aunde serikali inayoaminika kama alivyo yeye na wakikosea Mawaziri wake au taasisi zake alizoteua wakurugenzi wake basi ni kuwa serikali yake imeshindwa.

Hii ndiyo matokeo ya tafiti za REDET kama yalivyotolewa na Dr. Ndumbaro ikisema kuwa wananchi wanaamini serikali za mitaa kwa asilimia 42.2, Bunge (39.2), TACAIDS (35.4), Baraza la Mawaziri (33.8), Polisi (26.2), mahakama (23.8) na TRA (18.2).

Takwimu zingine ni kama PCB (18.1), Bodi ya mikopo (17.2), TANESCO (16.3) na TIC(10.5).

Takwimu hizi ziliendelea zaidi kwa kumlinganisha Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume kuwa Kikwete anakubalika kwa asilimia 67 nali Karume 47.8 tu.

Matokeo haya wanasema yalipatika baada ya kufanya utafiti kwa kuhoji watu huko Zanzibar na Tanzania Bara.

Hata pale Rais Kikwete mwenyewe alipogundua kuwa hana washauri, na hata wale aliowaweka kumshauri walikuwa wakitetemeka wanapofika kwake na kuchekacheka huku wakisifia kila jambo ndipo alipotamka kuwa hataki sifa za kinafiki ambazo Watanzania wengi wana utajiri wa sifa hata pale unapoharaibu.

Rais aliona nchi inaelekea pabaya huku washauri wake wakiwa hawana jipya wala hawamwamshi, na kila mara wakiimba nyimbo za sifa.

Lakini vilevile kwa mtazamo wangu hizi ni hadithi za sungura baada ya kushindwa kufikia tunda alilolitegemea na kusema ‘sizitaki mbichi hizi’ kama Rais alivyoiweka.

Je wasomi wa taaluma ya siasa ‘Political Science’ ni waimba kwaya wa Rais Kikwete au wapiga tarumbeta katika harusi za kitanzania wakati bwana na bibi harusi wakienda kuoana, sio kwa sababu wapiga tarumbeta wanapenda kutumia nguvu nyingi kupuliza, bali kwa sababu wanalipwa.

Je wasomi hawa wa siasa na asasi yao hii ya kutoa mafunzo ya demokrasia wanataka tuamini kuwa hata matatizo makubwa ya mgawanyiko wa kisiasa ambapo tumeona Wapemba wakitengwa na Serikali ya Zanzibar hata katika ajira, miundo mbinu na shughuli za kijamii, je wasomi wamechukua hatua endelevu au hatua pozeo tu?

Je wasomi wa kikundi hiki kilichojificha nyuma ya REDET wanajua kuwa kuna hila nyingi za siasa za kinafiki zinazofanyika Pemba na hata kudidimiza baadhi ya wasomi wa Pemba nali tukishuhudia fundi meli kutoka Pemba akipewa kazi ya kuakata tiketi za meli.



Moja ya mwandishi katika gazeti la kiingereza humu nchini ambaye makala yake yanagusa sana na kuibua uchokozi mzee Hilal Sued katika safu yake iitwayo Beyond the Boarder ya Gazeti la The African no. 2788.

Mzee Sued anasema utapeli umeongezeka ndani ya nchi ikitumia jina la Demokrasia, anajiuliza kuwa unaweza ukaamini kuwa wasomi wa chuo kikuu na asasi yao ya REDET wameanzisha chuo huko Zanzibar iitwayo Democracy Training College (DTC) ikiwa na lengo la kuwafundisha vijana wa Zanzibar juu ya ‘Political Tolerance (Uvumilivu wa Kisiasa)’.

Hii ina maana kwamba hawa wasomi wanataka watu wakae kimya bila kuulizauliza mambo hata utawala na sheria mbovu zinapopitishwa dhidi na hata pale demokrasia yao inapobakwa katika jina la demokrasia.

Tanzania inahitaji vyuo vingi vya demokrasia vinavyofundisha utawala bora, kuzuia rushwa na ufisadi na sio kufundisha vijana kunyamaza hata pale wanapohujumiwa, hawa ndio wasomi wetu.

Utakaaje kimya katika hali ya rushwa iliyokithiri, Chuo kama DTC ni vya kitapeli na hujuma mkubwa kwa Mtanzania na vizazi vyake na hizi hujuma vinaanzia Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam chini wa wasomi maprofesa na madaktari wa falsafa ya Siasa.

Ni Demokraisia gani inayotafitiwa na kufundishwa na REDET? Au tulijue moja kuwa hii ni asasi ya serikali ya awamu ya nne? Mtapumbaza watanzania mpaka lini na hii ni sehemu ya Chuo Kikuu chenye heshima na hadhi ya Kitaifa.

Wiki iliyopita siku ya jumamosi ya hii Januari katika mahafali ya kwanza ya chuo hicho kinachoendeshwa kupitia mpango wa REDET, Prof. Mukandala alisikika akivitaka vyama vya siasa na watendaji wa chuo hicho kupendekeza mada zitakazosaidia vijana kujenga demokrasia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Katika mahafali hayo jumla ya vijana 50 kutoka wilaya zote za Unguja na Pemba walihitimu mafunzo hayo ya ‘political tolerance’.

Mafunzo haya yalifadhiliwa na Norway, yalendeshwa na Idara ya siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Mpango wa Elimu ya Demokrasia (REDET).

Dhana ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar sio suala la elimu ya uraia, hapa tusiwadanganye Wapemba wala watu wa Unguja, sio suala la elimu.

Matatizo ya Zanzibar yanajulikana kabisa wala haiitaji tafiti nyingi wakati tunaiona CCM ikikalia kiti na haitaki kamwe chama tofauti na CCM ikiongoza kisiwa hicho.

Ni tamaa za kisiasa ndizo zinazoleta mpasuko na sio historia ya Zanzibar kama inavyosambazwa katika propaganda za nchi hii.

Suala la mpasuko wa kisiasa Zanzibar limejificha kwenye uchu wa madaraka kwa wana Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku wahifahidhina wa Karume na Rais Karume mwenyewe wakitumia blanketi la Muungano kuhujumu demokraisia katika kisiwa cha Zanzibar.

Wizi wa kura wakati wa uchaguzi, kauli mbaya katika majukwaa ya kisiasa, majigambo katika vyombo vya Habari na matumizi makubwa ya nguvu za kijeshi wakati wa uchaguzi hayakufanywa na vijana, yalifanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikipewa ushirikiano wa karibu kabisa na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vijana hawakuhusika kutuma jeshi kuleta vurugu Pemba na Darajani huku Unguja, vijana hawakupanga wizi wa kura, vijana hawapati nafasi ya kupanda kwenye majukwaa ya siasa na kutoa propaganda za kuleta uchochezi.

Kama ni kuanzisha chuo hiki, waliostahili kujiandikisha kusoma katika chuo hicho kinachoendeshwa na REDET ni Rais Abeid Amani Karume, Waziri Kiongozi wa Zanzibar Sham Vuai Nahodha na wengine kama akina Shamhuna na wafahidhina katika serikali ya Karume.

Maana ni hawa ndio chanzo cha vurugu za siasa Zanzibar, wasomi wa REDET wasiogope kukwepa ukweli kwa kukimbilia kufundisha vijana uvumilivu wakati nchi yao haiandaliwi mazingira mazuri ya mfumo endelevu wa kidemokrasia.

Chuo hicho kitatumia pesa nyingi bila kuleta faida yoyote ya maana, na hadi sasa tangu chuo hicho kuanzishwa ndio imetoa wahitimu 50, je hadi baada ya miaka mitano vijana waliohitimu hapo watakuwa wameleta mabadiliko ya kisiasa wakati masuala ya msingi hayajarekebishwa?

Karume anasema hayuko tayari kwa serikali ya mseto na hilo anasema kuwa ni ndoto, na akarudia kutamka kuwa mwenye hoja ya serikali ya mseto Zanzibar atoe.

Lakini huyu huyu ndiye aliyeifikisha Zanzibar kwenye vurugu hadi wapemba wakakimbilia shimoni huko Mombasa, kwani wapemba ni vichaa ambao hata kama haki ikitendeka katika uchaguzi wanaandamana au wanaleta vurugu, hata hivyo sijasikia REDET ikimwomba huyo Rais Karume kuhudhuria katika chuo hicho cha demokrasia, maana nadhani anakihitaji kuliko hawa vijana 50 waliohitimu.

Henry Kissinger aliyekuwa katibu wa nchi ya marekani aliwahi kuambiwa na wananchi wake pale alipotakiwa ashtakiwe kwa mauaji ya watu Vietnam, lakini watu wa chinichini katika serikali ndio waliokuwa wamekamatwa na kuhukumiwa hata ikafikia hatua akasema mwenyewe kuwa ‘sheria ni kama utando wa buibui ina nguvu nyingi kiasi cha kumnasa mtu mdhaifu na nguvu kidogo ya kumnasa mwenye nguvu (Law is like a web, it is too strong the hold the weak and too weak to hold the strong)’.

Ni suala la aibu sana msomi anapotumika katika harakati za kutekeleza mkakati wa kurubuni nchi.

Ni wazi kabisa kuwa msomi maarufu huyu Prof. Mukandala alisoma pamoja na Rais Jakaya Kikwete, ni rafiki yake na pia ni mshauri wake katika mambo ya siasa, hii ilikuwa ni nafasi nzuri kumsaidia Rais kwa mipanga endelevu za kujenga mfumo madhubuti wa kidemokrasia katika Tanzania na sio kusimika mfumo pozeo wa kutaka kurubuni vijana ambao ni wahusika wadogo wanaoingia katika fujo pale ambapo wanaona mambo yakifanyika ovyoovyo.

Kwa namna hii itafikia hatua hatuwaamini wasomi walio wengi na hasa wale wanaotumika katika kuendeleza propaganda za mojawapo ya chama au kutumika kupumbaza watanzania na vizazi vyao.

Asasi zitatumia pesa nyingi kufundisha vijana utawala bora na mambo mengi lakini suala linabaki palepale kuwa wakubwa wanaotoa mionozo ya kisiasa wasipotumia utawala bora na vijana hawatavumilia utawala mbovu na kuvumilia ni kujitia vitanzi katika kuendeleza demokrasia nchini.

Kwa mawasilano: 0715 551455


No comments: