Viva Wanahabari na Amanda Areopagitica!
Na Nyasigo Kornel
Baadhi ya wababe na watemi wa kisiasa waliojitokeza duniani kukandamiza Uhuru wa Habari (Areopagitica) kama Joen Larien, Kenneth Robert na Heleg Drugman walikuwa wakiamini kuwa ilikuwa ni salama mwananchi hasipopata Habari zile kali za ndani ya serikali kuliko akizifahamu, kwani waliamini kuwa wananchi wakizijua ilikuwa inawapunguzia wanasiasa uaminifu kwa wananchi wao.
Hii ndio maana katika miaka ya nyuma gazeti kama The Guardian na The Financial Times ya Uingereza hazikuandika kuhusu kero za wafanyakazi waliokuwa wakiteswa katika viwanda vya mabepari huko Uingereza.
Mbabe wa kisiasa dhidi ya Habari kama Joen Larien, Kenneth Robert na Heleg Drugman hapa kwetu ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo mheshimiwa Seif Khatib akiwa na muswada wake huo anaofikiri kuwa watanzania bado ni mazezeta.
Mbinu zinazotaka kutumiwa katika karne hii ya 21 na serikali yetu katika kukandamiza uhuru wa Habari nchini zilitumika Uingereza katika mwaka 1695 na hazikufanikiwa.
Ni katika kipindi hicho ndipo John Milton aliandika kauli kali kwelikweli ya kutetea uhuru wa Habari iitwayo Areopagitica (uhuru wa Habari) iliyopinga sheria ya Bunge la Uingereza wa kutaka Wahariri wapewe leseni maalumu na serikali ya nchi hiyo.
Sio muda mrefu wadau wa Sekta ya Habari walitoa tamko la kuikataa muswada wa uhuru wa vyombo vya Habari ambayo moja ya kipengele katika muswada huo ni kuanzisha kitengo kitakachothibitisha viwango vya wahariri wa vyombo vyote vya Habari kiitwacho Bodi ya Viwango ya Vyombo vya Habari (Media Standard Board- MSB).
Kihistoria vyombo vya Habari vimekuwa ni jukwaa ambalo wanyonge wamekuwa wakiitumia kuinua sauti zao hasa pale wanapotaka kuiwajibisha, kuikosoa na kuirekebisha serikali yao.
Katika harakati wa kutetea uhalali wa wananchi kupata Habari bila vikwazo gazeti la Chicago Times liliwahi kuandika na kuwa ni jukumu la magazeti kuchapisha Habari na kuibua changamoto, litakalotokea na liwe (It is a newspaper’s duty to print the news and raise hell).
Vyombo vyote vya Habari vinavyoipa changamoto serikali ni adui yao, tena adui namba moja.
Utajiuluza kuwa ni mhariri wa aina gani huyo atakayekubalika na chombo hiki serikali ambayo serikali yenyewe inataka ije iitumie kama kibaraka ya kuwakandamiza wahariri, na hasa wale wahariri wanaoipa serikali changamoto na kuruhusu makala nzito yenye hoja kuchapwa na gazeti lake?
Mhariri anayekubalika na serikali ni yule ambaye gazeti lake litatoka na Habari zinazosifia viongozi wa serikali au Habari zinazowakwepesha wasionekane wanawajibika na matatizo ya kijamii.
Kama wakati wa sakata lilioonekana kama kuna kila aina ya ufisadi yake, tena kuna viongozi mkono wa serikali ndani yake katika kuingiza mtambo wa kuongeza megawati za umeme 20 katika grid ya taifa iliyochukuliwa na Richmond, magazeti mengi yalikuwa yakimkwepesha Rais Jakaya Kikwete katika tuhuma zote.
Ukisoma magazeti mengi katika ukurasa wa mbele utaona maandishi makubwa yakiaandika kumficha Rais na kumtoa katika matatizo kama ‘Rais Kikwete adanganywa’, ‘JK apotoshwa kuhusu Richmond’, ‘JK adanganywa umeme wa Kusini’.
Kama Rais huyu ndiye aliyesema kuwa umeme wa Richmond wa megawati 100 utakuwa tayari mwezi wa tisa, akahairisha tena akasema mwezi wa kumi na moja, leo hii hajui itakuwa tayari lini, hasemi kabisa.
Huyu Rais yeye anadanganywa tu, huu sio ushabiki tu wa kisiasa? Yeye Rais anadanganywa na nani huyo? Kwa nini wahariri hujikuta wanakuwa sehemu ya ushabiki wa kisiasa? Kwa nini yeye ndiye anadanganywa kila siku katika mambo makubwa ya kitaifa? Huyo ni kiongozi wa aina gani wa kudanganywa kila mara?
Wahariri na wanahabari lazima tujikosoe kuwa tulimzoesha Rais wetu vibaya kwa kumwagia sifa kama malaika. Sasa baadhi ya watu walipoanza kutupa lawama kwa ile ile serikali iliokwishazoea kusifiwa ndio chanzo cha muswada huu ambayo hata nchi ya watu wenye upofu wa akili wasingeikubali.
Serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani vyombo vya Habari walikipigia debe, ukisoma kila ukurasa Rais Kikwete alikuwa akiandikwa kama vile Mesiah aliyekuja kuwakomboa wanyonge.
Kiongozi mchafu ndiye anayeogopa vyombo vya Habari. Kipindi kile kabla Rais Kikwete hajaboronga alikuwa akiwashawishi viongozi wa serikali yake kuwa karibu na vyombo vya Habari na kuwa wasiogope waandishi wa Habari.
Leo hii ukijitambulisha kuwa wewe ni mwandishi wa Habari katika ofisi ya serikali na hasa Wizara yenye kashfa, utaambiwa kuwa Waziri hayupo au kama yupo utaambiwa kuwa ana kikao.
Mwaka juzi Mwenyekiti wa Habari Corporation alipata misukosuko ya uraia kumbe chini ya uvungu ilikuwa ni siasa chafu ya baadhi ya watu ambao hupenda kumwagiwa sifa hata pale tunapokamuliwa tone la mwisho la damu.
Mwaka juzi hiyo hiyo nchini Uganda, Rais Mseveni aliamua kulifungia gazeti la the Monitor baada ya gazeti hilo kuibua ufisadi wake na hata mhariri wake Charles Onyango Oboo kuhamishwa Uganda kurudi Kenya.
Si hayo tu katika vyombo vya Habari na serikali, nchini Zimbabwe Gazeti la The Sunny lilifungiwa na hata mhariri wake kutishiwa maisha kila mara.
Ninaweza kusema kuwa ni nchini Kenya tu ndio naona vyombo vya Habari vikiwa na uhuru ule wa kiwango fulani zaidi ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika.
Na hii ni kwa sababu ya kuwa na vyama vya siasa vyenye sauti.
Swali la kujiuliza ni kuwa serikali itatumia kigezo gani kujua kuwa huyu mhariri ana kiwango na huyu hana kiwango.
Je watatumia viwango sahihi vya kitaaluma kama wanasheria wanavyofanya wanapowatahini mawakili wapya kwa kuwahoji maswali?
Uzoefu unaonyesha kuwa vijana wengi wanaosomea uandishi wa Habari hawapendi kuandika na hivyo wengi wao hupenda nafasi za Afisa Uhusiano katika mashirika na idara za Serikali.
Kwa sababu uandishi ni taaluma na sanaa, na kama sanaa zingine mpaka mtu awe anaipenda ndipo huweza kujituma kuandika maana kuandika sio kazi rahisi, utambulika kwa kuandika na sio kuonyesha cheti.
Kwa jinsi hiyo zaidi ya robo tatu ya wahariri Tanzania hawajasomea taaluma ya uhariri ila wameipata kupitia uzoefu kwa vitendo, na wanaifanya hiyo kazi vizuri.
Sasa serikali itatumia kigezo cha uhariri kama sanaa, uzoefu au kama taaluma?
Thomas Barnes mhariri aliyeipandisha kiwango cha juu sana gazeti maarufu sana duniani la The Times hakuwa na elimu kubwa, aliwahi kusoma middle school za enzi hizo tu na hakugusa masomo ya vyuoni. Pamoja na elimu yake ndogo na katika umri wa miaka 30 alikuwa amekabidhiwa medali 6 za mhariri bora nchini Uingereza katika miaka ya 1976.
Kama MSB lingekuwepo huko Uingereza unadhani mhariri aliyepta uhariri katika umri wa miaka 26 angepewa leseni kweli?
Mwingine kama huyo ni Cobbett aliyekuwa mhariri wa magazeti ya kila siku nchini Uingereza iitwayo Black Dwarf na Poor Man’s Guardian, yeye ndiye mwanzilishi na mhariri wa gazeti hilo akiwa ana umri wa miaka 28 tu baada ya kupata cheti katika masomo ya uchumi. Leo hii hata baada ya kifo chake Waingereza wanamwita baba wa waandishi.
Je hii MSB ikianzishwa itaweza kumwidhinisha mwanafunzi kutoka chuoni na cheti chake cha uchumi?
Mjerumani aliyewahi kupata tuzo mara nyingi la mhariri bora kuliko wote Ujerumani alikuwa anaitwa Rayner Degüs akiwa hana taaluma hiyo ya uandishi, hana shahada wala cheti chochote ya ujuzi wowote.
Baada ya kushindwa kusoma kwa kupoteza wazazi wake na mara baada ya maisha kuwa magumu aliamua kuandika makala za hasira zilizowezesha serikali ya Ujerumani kurekebisha sheria zake za ustawi wa jamii na kuanza kutunza watoto yatima kwa mahitaji yote.
Na huyu ndiye mwandishi wa kitabu cha uandishi wa Habari kiitwacho ‘Writer can change their cities’.
Serikali ina jeuri ipi ya kuwatambua watu kama hawa au kuwaondoa katika harakati zao!
Na ndio maana tunasema serikali isiwachezee watu akili kwa muswada kama huu ambao ungetakiwa uwepo kipindi kile watu wakiwa bado wamelala.
Ni vema serikali kujua kuendesha mambo yake kwamba tofauti na serikali za miaka ya 1970 ambapo unaweza kuzuia Habari.
Kwa kawaida kama mambo yameshawazidia serikali inayojiita wanamtandao wangerusha propaganda zao kwenye vyombo vyao vya Habari, wanavyo na wanaweza kuvitumia kudanganya na kupindua maneno.
Kiwango cha mhariri anayehitajika inaendana na mahitaji ya chombo chenyewe cha Habari, aina ya Habari inayoandikwa na chombo hicho na uwezo wa kumlipa aina ya mhariri huyo anayehitajika.
Serikali ina mambo mengi yaliyowashinda, na tayari wamekuwa wakiyalimbikiza kila leo, ndio maana wanakimbilia kufumba midomo ya vyombo vya Habari wasiseme kwa maana wataumbuka.
Ndio maana katika hotuba aliyotoa mwanaharakati wa kutetea haki ya wananchi kupata Habari kwenye mkutano wa wamiliki wa vyombo vya Habari aliwahi kusema ‘if you can’t beat ’em, join ’em but expect no changes(kama huwezi kuwashinda, ni afadhali uwaunge mkono, lakini usitegemee mabadiliko).
Katika nchi ambazo kuna hatua kubwa katika uhuru wa Habari hata vyombo vya Habari vya serikali zimeonekana vikiikosoa serikali yenyewe, kwa maana.
Miaka miwili nyuma serikali ya China ilifikia hatua ikataka kuiwekea vyombo vyake yenyewe masharti kwa maana ilikuwa ikipinga mambo ya kipuuzi inayofanywa na serikali yenyewe.
Na ndio pale tuliposikia malumbano makali kwenye magazeti ya serikali ya China kama Jen-Min Jih-Pao, The People Daily ya mjini Peking.
Sio hapo tu tumeona hata nchini India na Pakistan magazeti ya serikali ikiwajibisha na kuuliza viongozi juu ya mambo yenye mstakabali wa kitaifa, magazeti kama Dawn ya Karachi, The Hindu na Jang.
Leo hii serikali Waziri Seif khatib anataka mfumo wa utoaji wa Habari uwe kama ule wa vyombo vya Habari vya serikali!
Mwananchi ana haki ya kupata Habari, mwanahabari anayo haki ya kuhoji juu ya maswala muhimu yenye mstakabali wa jamii, na vyombo vya Habari wanayo haki ya kuzitoa kulingana na sera ya gazeti lenyewe, na kama kuna vizingiti basi ninasema Viva wanahabari na Amanda Areopagitica!
0715 551455
Saturday, January 13, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment