Friday, January 19, 2007
Miaka 48 ya Mijadala Isiyoisha
Miaka 48 ya mijadala ya EAC isiyoisha
Na Nyasigo Kornel
NI MIAKA arobaini na nane mjadala umekuwa ukiendelea sio tu kwa wananchi bali hata kwa viongozi waandamizi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC).
Aliyekuwa Waziri wa Biashara wa Kenya J.G. Kiano katika mwaka wa 1959 akitoa sababu tatu alizokuwa akiamini kabisa kuwa ingehatarisha shirikisho hilo.
Ilipofika 1963 Kano hakuona haja ya kuwepo kwa jumuiya hiyo kwani Kenya ilikuwa bado ipo mikononi mwa walowezi na hivyo alikuwa na wasiwasi kuwa walowezi hawa wangeweza kusambaza nguvu zao za kikoloni hadi Tanzania na Uganda hata kuzorotesha juhudi za kupigania uhuru kwa nchi hizo.
Hivyo katika tamko la mwaka huo 1963 mambo yalikuwa bado magumu sana hata kufikia hatua viongozi wakachagua maeneo ya kuyafanyia kazi kwa pamoja kama mipango ya kiuchumi, kutumia nguvu kazi kutoka katika nchi wanachama na sio kuwaleta kutoka nje ya nchi, kuanzisha benki la pamoja (central Bank), ulinzi na kuwepo na mwakilishi mmoja wa wa kidlomasia kwa nchi zote.
Hapa ni wazi kuwa viongozi waliondaa utaratibu huu walifikiri kuwa haya ndiyo maeneo sahihi na kwalo wangepunguza matumizi makubwa ya pesa na wangetumia pesa kidogo kukuza nguvu kazi kwa matumizi ya nchi wanachama.
Viongozi wa kipindi hiki walifikiri kuwa uchumi wa Tanzania, Kenya na Uganda ungekuwa kama wangetumia soko la watu wapatao milioni 25 katika nchi hizi kwa kipindi hicho nah ii ingeweza kuvutia wawekezaji wa nje na kuongeza tija katika mitaji ya wananchi wan chi hizi.
Ilifikiriwa kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ingeweza kuanza mwaka 1963 na hivyo kamati maalum ilipewa majukumu ya kuandaa mwelekeo wa katiba ya Jumuiya na ripoti yao iliwekwa wazi mbele ya mkutano uliofanyika mwezi Agosti ya mwaka huo 1963.
Aliyeanza kuguna na kutoa dukuduku la Jumuiya hiyo ni aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uganda wa kipindi hicho ni Dr. Milton Obote mnamo Octoba 1963, siku chache tu baada ya katiba kuwa imeandaliwa.
Obote alisema kuwa kuna mambo ya msingi ambayo Uganda lazima yaweke sawa kabla na baada ya kujiunga na jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki na kwa hali hiyo alipinga kuanzishwa kwa jumuiya hiyo katika mwaka 1963.
Mjadala haukuishia hapo, mwaka 1964 Tanzania pia ikawa imeona mwanya katika mchakato wa Jumuiya hiyo, na ndipo Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania Oscar Kambona naye alipoelezea mashaka yake juu ya shirikisho waliokuwa wameamua kujiunga kwa shingo upande.
Oscar Kambona alisema kuwa Tanzania ilipopata Uhuru mwaka 1961 waliona kuwa kuna haja la kuwa na soko la pamoja, sio kwa sababu Tanzania iliamini kuwa kuna usawa katika soko la pamoja lakini tuliamua kujiunga ili kutoa nafasi ya kuwepo kwa shirikisho hilo.
Baadaye baada ya kuchunguza kwa makini Kambona alitoa tamko kuwa hakukuwepo na haja ya kupuuza hasara ambazo Tanzania ingepata katika soko hilo la pamoja.
Na ilipofika mwezi machi 17 1964 Waziri wa Mipango na Maendeleo wa Tanganyika Nsilo Swai, katika kikao cha siri sana cha mipango ya uchumi kilichofanyika kule Entebbe-Uganda alisema kuwa nchi yake (Tanganyika) ilikuwa ikiporomoka kiuchumi na hivyo alitaka mwafaka ufikiwe haraka juu ya mjadala wa kuweka urari sawa wenye uwiano katika biashara na viwanda kwa nchi ya Uganda na Kenya dhidi ya Tanzania.
Nsilo Swai alisema kuwa njia sahihi ya kuleta uwiano sawa ni pamoja na kutumia njia ya kutoza ushuru mkubwa kwa bidhaa ya Kenya na Uganda zilizokuwa zikimiminika kuja Tanzania huku Tanzania ikiwa haina cha kuuza katika hilo soko la pamoja.
Ilipofika 1965 Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa Rais wa Tanzania alitoa hotuba iliyoleta iliyoshtua shirikisho hilo pale aliipoimbia Mkutano mkuu wa Sheria kuwa Tanzania inatambua usumbufu ambao sheria hiyo mpya ya ushuru ungeleta kwa nchi ya Kenya na Uganda na akasema kuwa amejitahidi kujizuia kuleta huo usumbufu lakini maji yamemfikia shingoni.
Mwalimu Nyerere alisema, "Ingawa tatizo hili lilikuwa wazi kwetu toka tulipopata uhuru lakini hatukuchukua hatua mpaka ilipofikia mwaka 1964, tulifikiri kuwa hili suala lingeweza kushughulikiwa katika mikakati ya jumuiya hii. Kwa muda mrefu tuliweza kuikubali hasara na upotevu wote kama gharama ya thamani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Lakini Ukimya huu haitoa njia mbadala bali na kuangalia namna ya kurekebisha urari wa kibiashara katika soko la pamoja. Kama mwafaka huu hautafikiwa leo basi tutajua tutakavyofanya kurekebisha mfumo huu wenyewe nje ya shirikisho."
Hii ilikuwa na maana kuwa Tanzania ilikuwa inakwenda kutoza ushuru kwa njia zake yenyewe bidhaa za Kenya na Uganda zinazoingia ndani ya nchi, na hii ingekuwa ni ukiukwaji wa maazimio ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mvutano huu ulifanya kuitishwa kwa mkutano wa wakuu wa nchi huko Nairobi Kenya Aprili 10 1964, ambapo Mawaziri wawili wa Tanzania Nsilo Swai na Oscar Kambona wa walikwenda kutetea hoja ya Tanzania juu ya kurekebisha sheria za ushuru ili kuweka urari sawa wa kibiashara, na hivyo kuwezesha Tanzania kuendele katika Umoja huo.
Ni katika mkutano huu ndipo hawa Mawaziri na wawakilishi walipotoa tamko kuwa Tanzania haikuwa na nia ya kujiondoa katika Shrikisho hilo bali kuangalia njia muafaka wa kutatua tatizo la urari wa kibiashara.
Katika mkutano huu wajumbe Tanzania walipopewa uhakika kuwa kamati ya dharura itaundwa kushughulikia matatizo ya biashara yaliyopo katika soko la pamoja katika nchi hizi tatu.
Kutokufurahi kwa wajumbe wa Kenya katika mkutano huo haukuwa wazi mpaka baadaye kidogo katika baadhi ya taarifa zao zilizoletwa kwa ajili ya hiyo jumuiya, itakumbukwa kuwa Kenya ni nchi iliyokuwa ikifaidika sana na Jumuiya hii na sasa siri ya mafanikio yao ilikuwa imewekwa wazi.
Hasira na masikitiko hayo yalionekana waziwazi usoni kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo wa Kenya Jomo Kenyatta na pia mwenyekiti wa Mkutano mkuu wa viongozi wa nchi wanachama.
Kenyatta alifungua mkutano akisema, "Mkutano umeitishwa ili kujadili uamuzi wa Serikali ya Tanganyika kutaka kujiondoa katika soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki."
Aliendelea kusema, "Hapa kwetu Kenya tumesikitishwa na uamuzi huo. Ingawa katika urari wa biashara Kenya ndio inayofaidika zaidi, lakini hatujutii kwa sababu kufaidika kwetu sio kwa kutumia mgongo wan chi nyingine bali ni kwa sababu ya bidii yetu, na tunasikitika kuwa hatutafanikiwa zaidi iwapo Tanzania itajiondoa katika soko la pamoja ingawaje hata wao wanayo mengi wanayofaidika nayo kutoka katika shirikisho."
Jomo Kenyatta aliendelea kuweka msimamo wake akisema kuwa kama ni vigumu kuwepo na soko la pamoja basi mpango huo wa soko hilo lingehairishwa mpaka mwaka uliofuatia kwani alijitetea kuwa hata wao walikuwa wamepata uhuru muda mchache tu na walikuwa na matatizo mengi hasa ya ajira kwa watu wao.
Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwepo katika huu mjadala alikuwa akimsikiliza sana Jomo Kenyatta aliinuka na kuanza kwa kukosoa kauli ya Jomo Kenyatta.
"Mwenyekiti umesema wakati wa ufunguzi wa kikao hiki kuwa Tanganyika imefikiwa uamuzi wa kujiondoa katika soko la pamoja la Jumuiya Afrika Mashariki. Naomba nikukosoe kwa kauli yako hiyo. Tanzania ilileta mswada wake ili baadhi ya miundo iliyopo katika biashara na viwanda iweze kurekebishwa. Na hii ni suala rahisi sana na wala haitaji akili kubwa sana, na haihusiani na kujiondoa katika jumuiya."
Mwalimu Nyerere alisema kuwa hakuna mtu wa kulaumiwa au kumsifiwa kwa matatizo na mafanikio yua soko la pamoja kwa maana matatizo mengine tumeyarithi kwa muundo wa uchumi wa kikoloni.
Mwalimu Nyerere alisema, "Watu wote walosoma uchumi wa pamoja wanasema kuwa hakuna Jumuiya ya Afrika mashariki bila soko la pamoja kwani tayari jumuiya imeshapata viwanda, miundombinu na miradi."
Itakumbukwa kuwa Kenya ilikuwa imefika mbali katika biashara na viwanda kwani walipopata uhuru kutoka kwa wale wazungu walowezi tayari sehemu kubwa ya miundo mbinu za kiuchumio iliitanguliza nchi hiyo mbele ya nchi zote za Afrika ya Mashariki, na hivyo hili soko la pamoja lilishabikiwa na Kenya kwa ajili ya maslahi yake.
Kenya na Uganda ilikuwa inauza vitu vyao vingi huku Tanganyika kuliko ilivyouza Tanganyika ikiuza kwao.
Njia sahihi kwa Tanganyika ilikuwa ni kuwa kulinda soko lake kwa kiwango fulani kwa kutoza ushuru kwa bidhaa kutoka nchi wanachama nah ii ingeiumiza Kenya ambayo tayari Tanzania ni soko lake.
Katika mwisho wa mkutano huo aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uganda Dr. Apollo Milton Obote alisema kuwa hata Uganda walifikiri kuwa Tanganyika ilikuwa ikitaka kujiengua kutoka katika soko hilo la pamoja, na hivyo akasisitiza tamko la Mwalimu Nyerere lishughulikiwe haraka sana.
Ni katika Mei 15 1965 ndipo Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipopata pigo nyingine ambayo iliikuwa ya silaha kutoka nchini China iliyokuwa imesheheneshwa kwenye magari ya mzigo kutoka Tanzania kuelekea nchini Uganda.
Mashehena haya yalikamatwa mjini Kisii Kenya karibu na mpaka wa Tanzania, Kenya na Uganda.
Mashehena haya yalipochunguzwa ilikutikana imebeba tani 75 ya silaha kutoka nchini China nail ikiwa na watu 45 waliokuwa wkiisindikiza msafara huo wa mashehena yenye silaha ambapo walikuwepo maaskari waliovaa nguo za jeshi la wananchi la Uganda na dereva aliyekuwa raia.
Ilipofika Mei 21 ya mwaka huo 1965 Serikali ya Uganda na Tanzania walitishia kuondoka katika soko la pamoja la Afrika Mashariki hadi pale serikali ya Kenya itakapoachilia yale mashehena yenye silaha. Suala hili lilimalizwa kiurafiki.
Makubaliano yale yaliyofanyika Nairobi ya kuandaa kamati ya dharura kama njia nzuri itayoleta urari katika biashara ilipokuwa tayari ilizaa Makubaliano ya Kampala mwaka 1964 (The Kampala Agreement 1964) ambapo viongozi 3 wa nchi zote za umoja huo walikuwepo.
Katika Makubaliano ya Kampala, ripoti ilitoa mapendekezo ya namna nzuri ya kuleta urari sawa wa biashara katika nchi hizi tatu.
Kwanza kabisa ili kuongeza urari sawa walitoa pendekezo kuwa makampuni yale ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanya kazi katika nchi zaidi ya mbili yaongeze uzalishaji kwa kiwango kikubwa katika nchi yenye upungufu katika urari wa biashara.
Walitoa pendekezo lingine kuwa viwanda vilivyorundikana Kenya visambaze matawi yake kwa nchi ya Tanzania na Uganda na vilevile viwanda vipya vitavyojengwa viweze kujengwa Uganda na Tanzania.
Vilevile ilipendekezwa kuwa kuwepo na mfumo utakaoruhusu nchi inayozalisha sana kusafirisha kwa nchi wanachama biashara zake kwa viwango vinavyowiana ili nchi yenye upungufu iweze kuzalisha ziada na kwa faida.
Na zaidi ilipendekezwa kuwa mgawanyo wa viwanda iwe sawa kwa nchi zote wanachama.
Na kwa wakati huu maamuzi ya haraka ilichukuliwa ili kukinusuru umoja na ndipo waziri wa Biashara alipotangaza kuwa viwanda baadhi ya viwanda vilivyotakiwa kufanya kazi katika nchi hizi zote na hasa Tanzania na Uganda ili kuongeza uzalishaji kama vile Kiwanda cha tumbaku, kiwanda cha viatu cha bata, Kampuni ya bia ya Afrika Mashariki na British Standard Portland Cement (Bamburi).
Haya yote yalikuwa ni katika kutafuta urari wa kibiashara ili nchi zote wanachama waweze kufaidika na soko la pamoja nah ii ingepunguza kupwaya kwa Tanzania na Uganda katika biashara zake kwa asilimia 25 na kufanya Tanzania na Uganda kutofautiana kwa asilimia moja.
Ni wakati huu ilipokubalika kuwa tuwe na sarafu na noti ya aina moja kwa nchi zote za umoja huo.
Makubaliano ya haya ya Kampala yalitoa ubainisho wa bidhaa za Afrika Mashariki (East Africa Commodity) zilizokuwa zikitengenezwa na viwanda vilivyomilikiwa na shirikisho na bidhaa za ndani ya nchi (national Commodity) na hivyo kuleta mfumo wa kuhamisha kodi (Transfer tax in the EAC).
Hii ndio mara ya kwanza makubaliano haya yalipofanya mkakati wa makusudi kuleta urari wa biashara katika jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa bahati mbaya, Kenya haikukubaliana na mfumo huu na hawakutoa sababu ya kuikataa na hivyo makubaliano haya yakafia kwenye maandishi ya wino.
Tanzania na Uganda walichukulia hatua ya Kenya kukataa kama ni msumari wa mwisho katika jeneza la lililokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hatimaye Jumuiya hii ilianzishwa mwaka 1967 ilisambaratika mwaka 1977, pamoja na sababu nyingi za utofauti wa kisiasa kati ya viongozi wanachama akiwemo Rais wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Idd Amin Dada aliyekuwa Rais wa Uganda.
Hata hivyo baada ya kusambaratika viongozi waliona umuhimu wa kuanzisha tena Shirikisho la Afrika Mashariki na mnamo Julai 2000 ambapo mkataba mpya wa Uhuru wa Biashara ulisahiniwa mjini Arusha Tanzania.
Kenya ambayo ni nchi tajiri kwa hawa wanachama atalipia kodi kwa bidhaa zake zinazoingia Tanzania na Uganda kwa kiwango kinachopungua hadi kufikia mwaka 2010 ambapo ushuru wa pamoja itakapotozwa kwa nchi wanachama.
Katika Afrika mkataba wa shirikisho mpya inategemewa kuwepo na pesa ya aina moja itakayojulikana kama Shilingi ya Afrika ya Mashariki hadi kufikia mwaka 2009.
Moja ya mipango mingine iliyopo ni kuwa na soko la pamoja, visa na umoja wa kisiasa ambapo kutakuwepo na Rais wa Shirikisho na Bunge la pamoja hadi kufikia 2010.
0715 551 455
http://nyasigo.blogspot.com
emmakornel@yahoo.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment