Saturday, January 13, 2007

Viva

Viva Wanahabari na Amanda Areopagitica!

Na Nyasigo Kornel


Baadhi ya wababe na watemi wa kisiasa waliojitokeza duniani kukandamiza Uhuru wa Habari (Areopagitica) kama Joen Larien, Kenneth Robert na Heleg Drugman walikuwa wakiamini kuwa ilikuwa ni salama mwananchi hasipopata Habari zile kali za ndani ya serikali kuliko akizifahamu, kwani waliamini kuwa wananchi wakizijua ilikuwa inawapunguzia wanasiasa uaminifu kwa wananchi wao.

Hii ndio maana katika miaka ya nyuma gazeti kama The Guardian na The Financial Times ya Uingereza hazikuandika kuhusu kero za wafanyakazi waliokuwa wakiteswa katika viwanda vya mabepari huko Uingereza.

Mbabe wa kisiasa dhidi ya Habari kama Joen Larien, Kenneth Robert na Heleg Drugman hapa kwetu ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo mheshimiwa Seif Khatib akiwa na muswada wake huo anaofikiri kuwa watanzania bado ni mazezeta.

Mbinu zinazotaka kutumiwa katika karne hii ya 21 na serikali yetu katika kukandamiza uhuru wa Habari nchini zilitumika Uingereza katika mwaka 1695 na hazikufanikiwa.

Ni katika kipindi hicho ndipo John Milton aliandika kauli kali kwelikweli ya kutetea uhuru wa Habari iitwayo Areopagitica (uhuru wa Habari) iliyopinga sheria ya Bunge la Uingereza wa kutaka Wahariri wapewe leseni maalumu na serikali ya nchi hiyo.

Sio muda mrefu wadau wa Sekta ya Habari walitoa tamko la kuikataa muswada wa uhuru wa vyombo vya Habari ambayo moja ya kipengele katika muswada huo ni kuanzisha kitengo kitakachothibitisha viwango vya wahariri wa vyombo vyote vya Habari kiitwacho Bodi ya Viwango ya Vyombo vya Habari (Media Standard Board- MSB).

Kihistoria vyombo vya Habari vimekuwa ni jukwaa ambalo wanyonge wamekuwa wakiitumia kuinua sauti zao hasa pale wanapotaka kuiwajibisha, kuikosoa na kuirekebisha serikali yao.

Katika harakati wa kutetea uhalali wa wananchi kupata Habari bila vikwazo gazeti la Chicago Times liliwahi kuandika na kuwa ni jukumu la magazeti kuchapisha Habari na kuibua changamoto, litakalotokea na liwe (It is a newspaper’s duty to print the news and raise hell).
Vyombo vyote vya Habari vinavyoipa changamoto serikali ni adui yao, tena adui namba moja.

Utajiuluza kuwa ni mhariri wa aina gani huyo atakayekubalika na chombo hiki serikali ambayo serikali yenyewe inataka ije iitumie kama kibaraka ya kuwakandamiza wahariri, na hasa wale wahariri wanaoipa serikali changamoto na kuruhusu makala nzito yenye hoja kuchapwa na gazeti lake?

Mhariri anayekubalika na serikali ni yule ambaye gazeti lake litatoka na Habari zinazosifia viongozi wa serikali au Habari zinazowakwepesha wasionekane wanawajibika na matatizo ya kijamii.

Kama wakati wa sakata lilioonekana kama kuna kila aina ya ufisadi yake, tena kuna viongozi mkono wa serikali ndani yake katika kuingiza mtambo wa kuongeza megawati za umeme 20 katika grid ya taifa iliyochukuliwa na Richmond, magazeti mengi yalikuwa yakimkwepesha Rais Jakaya Kikwete katika tuhuma zote.

Ukisoma magazeti mengi katika ukurasa wa mbele utaona maandishi makubwa yakiaandika kumficha Rais na kumtoa katika matatizo kama ‘Rais Kikwete adanganywa’, ‘JK apotoshwa kuhusu Richmond’, ‘JK adanganywa umeme wa Kusini’.

Kama Rais huyu ndiye aliyesema kuwa umeme wa Richmond wa megawati 100 utakuwa tayari mwezi wa tisa, akahairisha tena akasema mwezi wa kumi na moja, leo hii hajui itakuwa tayari lini, hasemi kabisa.

Huyu Rais yeye anadanganywa tu, huu sio ushabiki tu wa kisiasa? Yeye Rais anadanganywa na nani huyo? Kwa nini wahariri hujikuta wanakuwa sehemu ya ushabiki wa kisiasa? Kwa nini yeye ndiye anadanganywa kila siku katika mambo makubwa ya kitaifa? Huyo ni kiongozi wa aina gani wa kudanganywa kila mara?

Wahariri na wanahabari lazima tujikosoe kuwa tulimzoesha Rais wetu vibaya kwa kumwagia sifa kama malaika. Sasa baadhi ya watu walipoanza kutupa lawama kwa ile ile serikali iliokwishazoea kusifiwa ndio chanzo cha muswada huu ambayo hata nchi ya watu wenye upofu wa akili wasingeikubali.

Serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani vyombo vya Habari walikipigia debe, ukisoma kila ukurasa Rais Kikwete alikuwa akiandikwa kama vile Mesiah aliyekuja kuwakomboa wanyonge.

Kiongozi mchafu ndiye anayeogopa vyombo vya Habari. Kipindi kile kabla Rais Kikwete hajaboronga alikuwa akiwashawishi viongozi wa serikali yake kuwa karibu na vyombo vya Habari na kuwa wasiogope waandishi wa Habari.

Leo hii ukijitambulisha kuwa wewe ni mwandishi wa Habari katika ofisi ya serikali na hasa Wizara yenye kashfa, utaambiwa kuwa Waziri hayupo au kama yupo utaambiwa kuwa ana kikao.

Mwaka juzi Mwenyekiti wa Habari Corporation alipata misukosuko ya uraia kumbe chini ya uvungu ilikuwa ni siasa chafu ya baadhi ya watu ambao hupenda kumwagiwa sifa hata pale tunapokamuliwa tone la mwisho la damu.

Mwaka juzi hiyo hiyo nchini Uganda, Rais Mseveni aliamua kulifungia gazeti la the Monitor baada ya gazeti hilo kuibua ufisadi wake na hata mhariri wake Charles Onyango Oboo kuhamishwa Uganda kurudi Kenya.

Si hayo tu katika vyombo vya Habari na serikali, nchini Zimbabwe Gazeti la The Sunny lilifungiwa na hata mhariri wake kutishiwa maisha kila mara.

Ninaweza kusema kuwa ni nchini Kenya tu ndio naona vyombo vya Habari vikiwa na uhuru ule wa kiwango fulani zaidi ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika.

Na hii ni kwa sababu ya kuwa na vyama vya siasa vyenye sauti.

Swali la kujiuliza ni kuwa serikali itatumia kigezo gani kujua kuwa huyu mhariri ana kiwango na huyu hana kiwango.

Je watatumia viwango sahihi vya kitaaluma kama wanasheria wanavyofanya wanapowatahini mawakili wapya kwa kuwahoji maswali?

Uzoefu unaonyesha kuwa vijana wengi wanaosomea uandishi wa Habari hawapendi kuandika na hivyo wengi wao hupenda nafasi za Afisa Uhusiano katika mashirika na idara za Serikali.

Kwa sababu uandishi ni taaluma na sanaa, na kama sanaa zingine mpaka mtu awe anaipenda ndipo huweza kujituma kuandika maana kuandika sio kazi rahisi, utambulika kwa kuandika na sio kuonyesha cheti.

Kwa jinsi hiyo zaidi ya robo tatu ya wahariri Tanzania hawajasomea taaluma ya uhariri ila wameipata kupitia uzoefu kwa vitendo, na wanaifanya hiyo kazi vizuri.

Sasa serikali itatumia kigezo cha uhariri kama sanaa, uzoefu au kama taaluma?

Thomas Barnes mhariri aliyeipandisha kiwango cha juu sana gazeti maarufu sana duniani la The Times hakuwa na elimu kubwa, aliwahi kusoma middle school za enzi hizo tu na hakugusa masomo ya vyuoni. Pamoja na elimu yake ndogo na katika umri wa miaka 30 alikuwa amekabidhiwa medali 6 za mhariri bora nchini Uingereza katika miaka ya 1976.

Kama MSB lingekuwepo huko Uingereza unadhani mhariri aliyepta uhariri katika umri wa miaka 26 angepewa leseni kweli?

Mwingine kama huyo ni Cobbett aliyekuwa mhariri wa magazeti ya kila siku nchini Uingereza iitwayo Black Dwarf na Poor Man’s Guardian, yeye ndiye mwanzilishi na mhariri wa gazeti hilo akiwa ana umri wa miaka 28 tu baada ya kupata cheti katika masomo ya uchumi. Leo hii hata baada ya kifo chake Waingereza wanamwita baba wa waandishi.

Je hii MSB ikianzishwa itaweza kumwidhinisha mwanafunzi kutoka chuoni na cheti chake cha uchumi?

Mjerumani aliyewahi kupata tuzo mara nyingi la mhariri bora kuliko wote Ujerumani alikuwa anaitwa Rayner Degüs akiwa hana taaluma hiyo ya uandishi, hana shahada wala cheti chochote ya ujuzi wowote.

Baada ya kushindwa kusoma kwa kupoteza wazazi wake na mara baada ya maisha kuwa magumu aliamua kuandika makala za hasira zilizowezesha serikali ya Ujerumani kurekebisha sheria zake za ustawi wa jamii na kuanza kutunza watoto yatima kwa mahitaji yote.

Na huyu ndiye mwandishi wa kitabu cha uandishi wa Habari kiitwacho ‘Writer can change their cities’.

Serikali ina jeuri ipi ya kuwatambua watu kama hawa au kuwaondoa katika harakati zao!

Na ndio maana tunasema serikali isiwachezee watu akili kwa muswada kama huu ambao ungetakiwa uwepo kipindi kile watu wakiwa bado wamelala.

Ni vema serikali kujua kuendesha mambo yake kwamba tofauti na serikali za miaka ya 1970 ambapo unaweza kuzuia Habari.

Kwa kawaida kama mambo yameshawazidia serikali inayojiita wanamtandao wangerusha propaganda zao kwenye vyombo vyao vya Habari, wanavyo na wanaweza kuvitumia kudanganya na kupindua maneno.

Kiwango cha mhariri anayehitajika inaendana na mahitaji ya chombo chenyewe cha Habari, aina ya Habari inayoandikwa na chombo hicho na uwezo wa kumlipa aina ya mhariri huyo anayehitajika.

Serikali ina mambo mengi yaliyowashinda, na tayari wamekuwa wakiyalimbikiza kila leo, ndio maana wanakimbilia kufumba midomo ya vyombo vya Habari wasiseme kwa maana wataumbuka.

Ndio maana katika hotuba aliyotoa mwanaharakati wa kutetea haki ya wananchi kupata Habari kwenye mkutano wa wamiliki wa vyombo vya Habari aliwahi kusema ‘if you can’t beat ’em, join ’em but expect no changes(kama huwezi kuwashinda, ni afadhali uwaunge mkono, lakini usitegemee mabadiliko).

Katika nchi ambazo kuna hatua kubwa katika uhuru wa Habari hata vyombo vya Habari vya serikali zimeonekana vikiikosoa serikali yenyewe, kwa maana.

Miaka miwili nyuma serikali ya China ilifikia hatua ikataka kuiwekea vyombo vyake yenyewe masharti kwa maana ilikuwa ikipinga mambo ya kipuuzi inayofanywa na serikali yenyewe.

Na ndio pale tuliposikia malumbano makali kwenye magazeti ya serikali ya China kama Jen-Min Jih-Pao, The People Daily ya mjini Peking.

Sio hapo tu tumeona hata nchini India na Pakistan magazeti ya serikali ikiwajibisha na kuuliza viongozi juu ya mambo yenye mstakabali wa kitaifa, magazeti kama Dawn ya Karachi, The Hindu na Jang.

Leo hii serikali Waziri Seif khatib anataka mfumo wa utoaji wa Habari uwe kama ule wa vyombo vya Habari vya serikali!

Mwananchi ana haki ya kupata Habari, mwanahabari anayo haki ya kuhoji juu ya maswala muhimu yenye mstakabali wa jamii, na vyombo vya Habari wanayo haki ya kuzitoa kulingana na sera ya gazeti lenyewe, na kama kuna vizingiti basi ninasema Viva wanahabari na Amanda Areopagitica!

0715 551455

AFRICA


Afrika inavyodharaulika na wazungu

Na Nyasigo Kornel


Afisa mmoja wa Marekani aliyekuwa akisimamia misaada inayolewa na nchi hiyo kwa nchi za Afrika aliwahi kuongea kwa majigambo akisema kuwa ‘Principle export of the United States to Africa is money (bidhaa kubwa anayoisafirisha Marekani kuja Afrika ni pesa)’.

Kuna kikundi cha wazungu wanaofikiri kuwa Afrika ikinyimwa misaada na nchi tajiri inaweza ikapukutika na kupotea katika ramani ya viumbe hai wa dunia hii.

Katika kitabu chake Jacob Akol kiitwacho Burden of Nationality (Mzingo wa Uzalendo) aliwajibu wazungu hawa wanaoidharau Afrika akiwaambia kuwa Afrika itaendelea kuwepo hata ikifungwa milango yote ya misaada kwa maana misaada hiyo anayoiimanisha haimwinui mwafrika kwa lolote bali na kumdhalilisha na umjengea akili tegezi.

Historia ya biashara ya utumwa, ukoloni na misaada wanayotupatia wazungu imekuwa ikipumbaza viongozi wetu na kuwafanya vibaraka wa wazungu, makampuni yao na sera zao. Na zaidi zimemfanya mtu mweusi apoteze dira na kujidharau mbele ya mzungu.

Moja ya kikundi kilichojikita katika kulichukia sana watu weusi kiitwacho ‘anti-blacks’ huko Ulaya Magharibi hasa katika nchi za Italia, Hispania, Ujerumani na baadhi kutoka Uingereza na Marekani walikuwa wakijiuliza maswali kwenye vyombo vya Habari kuwa “Kwani Afrika ni nini kwetu mpaka tuisaidie? Kwa nini Afrika isiachwe ife na ikapotea katika ramani?”

Wazungu hawa nao walikuwa na hoja, walikuwa wakisema kuwa Afrika ina mali asili nyingi sana na wasomi sasa walikuwa wameongezeka kwa kiasi kikubwa, lakini ilikuwa haiwezi kuzalisha hata chakula chake.

Katika gazeti la Marekani iitwayo Time-Warner ilidiriki kuandika kuwa chakula kinachozalishwa katika ukanda wa mahindi wa kule Marekani ni kubwa kuliko mahindi inayozalishwa Afrika nzima na visiwa vyake. Na hivyo aliwahi kuishauri Marekani kutoa chakula cha ng’ombe ili igawanywe katika nchi zenye njaa barani Afrika.

Mwingine aitwaye Jamie Glazov katika kitabu chake aliyoiandika ya White Guilt alisema kuwa Afrika ikiendelea kuishi itachangia kuenena kwa kasi kwa magonjwa yanayotibika na hasa katika nchi za tropiki, kwa sababu serikali zao haziwezi kudhibiti hata ugonjwa unaotibiwa kwa senti moja ya Marekani.

Katika gazeti la Serikali la Ufaransa liitwalo Le Monde mwandishi wake mwenye asili ya Poland aitwaye Krzysztof Crosstie aliandika makala ikiuliza juu ya uwezo wa kufikiri wa Mwafrika na akaendelea kuuliza kama kweli Mungu alimuumba mzazi mmoja Adam na Eva. Alikataa na akasema kuwa anaamini katika mabadiliko ya maumbile kama anavyoeleza Charles Darwin katika nadharia yake ya mabadiliko katika maendelao ya binadamu.

Kuna baadhi ya machapisho ambayo yamekuwa yakitolewa na wazungu kukejeli Uafrika kila mara na kuonyesha kuwa Uafrika ni nusu ya maumbile na kuwa ndiye kiumbe aliyekaribu na nyani katika mtiririko wa maumbile.

Baadhi ya machapisho hayo ni kama vile The Missing Link, Racial Blasphemies, Black Rood, Ambiguous Identity, The Black Batch, A Thief In Babylon, White Guilt, Is your Father Black na Black Lies- White Lies. .

Kumekuwepo hata na midahalo ya kujadiliana iliyoendeshwa na gazeti la Readers Digest juu ya bara ipi yenye watu wenye uwezo wa juu wa kufikiri, mara nyingi Afrika anakokaa mtu mweusi imekuwa ikiwekwa ya mwisho katika fikra.

Ubabe huu wa kutaka kuingiza katika akili zetu kuwa sisi ni wajinga na watu dhaifu na wa chini hauishii hapo tu.

Michael Paul Rogin anaandika katika kitabu chake kiitwacho Black Face, White noise akisema kuwa waandaaji wa picha za sinema wa Holywood ambao wengi walikuwa ni Wamarekani wenye asili ya Kiyahudi walikuwa wakimdharau Mwafrika na hata kumwonyesha kama kiumbe dhaifu asiyestahili kiakili na hata kutendewa haki.

Baadhi ya sinema zinazomwonyesha mtu mweusi kama kiumbe kisichofaa ni kama vile ‘Gone with the Wind, Pinky, Home of Brave, Intruder in the Dust, The Jazz Singer and Whoopee’.

Na hata hivyo picha nyingi za high-tech utawakuta wazungu wa Holywood wakichaguana wao kwa wao na akiwepo mtu mweusi anakuwa ni chambo au mtu wa kutafutwa na ule mtambo, ili mradi tu ionekane kuwa mtu mweusi ni dhaifu na kuwa mzungu ashindwi.

Ni mpaka muda wa hivi karibuni ndio mwandishi kama Osca aliyeandika sinema ‘Crash’ iliyochezwa na Robert Jensen alipopewa zawadi ya kwa kuandika sinema iliyotoa taswira nzuri ya mtu mweusi.

Siku sio nyingi nilikuwa nikisoma mahojiano ya moja wa mawaziri wa zamani wa Rais Kabila alipokwenda Marekani katika gazeti moja liitwalo The Economist, badala ya mwandishi yule kumuuliza Waziri huyu alichokifuata Marekani, aliuza kuwa msaada gani unaotegemea kuupata kutoka hapa Marekani!

Wamarekani wanaamini kuwa viongozi wetu wakienda kule kwao wamekwenda kuombaomba au kutafuta msaada.

Ndio maana tuna jukumu la kuwauliza viongozi wetu kama Afrika imechoka kiasi hicho cha kujulikana na kama ombaomba, je Afrika bila msaada hata ya shilingi moja ya wazungu itapotea katika ramani? Na hiyo misaada imefanya nini kutufutia aibu ya kudharauliwa?

Sio siku nyingi mchezaji wa Barcelona- Hispania anayetoka Afrika aitwaye Samwel Eto alikuwa akizomewa na wazungu na kuonyeshwa kuwa anafanana na nyani, je wazungu wanapata jeuri wapi kama sio sisi ndio tunawapa penyo hizo?

Siku moja katika miaka ya nyuma niliporudi likizo nyumbani kijijini kutoka chuoni hapa Dar es Salaam, mzee mmoja aliyestaafu kazi baada ya kufanya kazi kama Afisa Elimu wa Wilaya wakati wa Mwalimu Nyerere aliniuliza kama ninaweza kujuana na mzungu yeyote ili nimuunganishe naye aweze kumwandikia kwa maana alikuwa akipata shida ya kuwalipia watoto watano ada ya shule katika shule za binafsi.

Hata nilipojaribu kumkwepa maana sikupenda ampe mzungu mtazamo huu ambao umekuwa ukitudhalilisha sana, alizidi kuniuliza kila siku kuwa, “Wewe kijana umesoma shule za seminari, ulikuwa ukifundishwa na wazungu, huna rafiki hata mmoja unipe niwasiliane naye! Wewe kijana ulikuwa unachezea bahati!”

Sasa huyu mzee ni Afisa Elimu hana malengo ya namna ya kutumia sehemu yake ya akili iliyobaki kubuni miradi midogomidogo, muda wote katika maono yake anamwona tu mzungu kama mkombozi wake na wala sio fikara zake.

Kijana mmoja aliyekuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliwahi kupata anwani ya barua pepe ya mzungu na kuanza kuwasiliana naye kwenye, alichokifanya huyu kijana wa chuo kikuu ni kuanza kueleza shida alizokuwa akitaka msaada wa kipesa, kumbe hakujua kuwa aliyekuwa anawasiliana naye ni mtoto mdogo wa miaka sita alyekuwa akisoma hatua ya pili huku nchini kwao.

Wazazi wa yule mtoto walimwandikia huyu kijana wa chuo kikuu kulaani hatua hiyo ya kumwomba mtoto mdogo wa miaka sita pesa.

Wa tatu kama ni mchungaji wa kanisa moja changa linaloendesha kazi zake hapa mjini Dar es Salaam, amesajili kanisa lake linalohubiri wokovu. Siku moja alilazimika kumsaidia mzungu kubeba mabegi ile mikubwa wakiwa wanatafuta tiketi ya yule mzungu aliyetaka kusafiri kwenda Mafia, walizunguka kwa masaa matatu.

Mwishoni baada ya usafiri wa siku ile kushindikana alimwomba yule mzungu kwenda kulala kwake, na baada ya pale waliachiana anwani na hivi karibuni alikuwa akitoa ushuhuda jinsi Mungu alivyomsaidia kumkutanisha na mtu ambaye sasa alikubali kumtumia dola mia kila mwezi.

Mzungu yule alifikiri kuwa mchungaji yule alikuwa akifanya wema kama mchungaji, kumbe wema anaouonyesha Mwafrika huyu dhaifu kwa mzungu ni kuwekeza.

Huu udhaifu auhishii hapo, nilipokuwa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, wazungu walikuwa wakija kwa awamu katika kozi fupi na nyingi zilikuwa ni masomo ya ‘arts’.

Vijana wengi walilazimika kujenga nao uhusiano hata kama haukuwatoka rohoni, walijitahidi kulazimisha kuongea kiingereza kwa matamshi yale ya kizungu ili mzungu ajisikie kuwa yeye hana utofauti na vijana wa kizungu.

Kwa kijana wa Kiafrika, na hasa walio wengi, na zaidi wasio na mwamko wa kifikira, wanaona kabisa kuwa kule kusalimiana na mzungu ni bahati na kulala naye kimapenzi ni suala la kutangaza na linaweza kumtenga hata na jamii yake kubwa ya Waafrika.

Katika masimulizi ya safari za James Bandrick alipotembelea mji wa Buhemba-Mara katika kipindi kile dhahabu zilipokuwa zikikusanywa na hao wazungu kupeleka kwao, mmoja ya familia kutoka katika jamii ya Wanata aliyoifikia, baba wa ile familia alilazimika kumwachia kitanda chake huyu mzungu na kisha yeye kulala chini kwenye ngozi sakafuni na mke wake.

Safari yake ilichukua wiki mbili, aliwasifu Waafrika kwa ukarimu, na alifikiri alikuwa amewajua Waafrika walivyo, siku ya mwisho alipokuwa anaondoka, aliangalia kwenye sanduku hakuona viatu, baadhi ya pesa, nguo na hata vitu vingine vya thamani vilikuwa vimeibwa.

Mwishoni alikiri kuwa ni vigumu kumfahamu Mwafrika kwa siku moja, kwa maana wema wao hauwatoki rohoni, kwetu wema ni tendo la mazoea na mila wala haionyeshi undani wa Mwafrika. Kwani hata unaweza kukaribishwa kula chakula kama tendo la mazoea na ukisha kula na kuondoka wakakusema.

Mama mmoja wa Kitanzania alikuwa ameolewa na Mjerumani na alikuwa akiishi naye mjini Dar es Salaam, siku ilipofika ya kwenda kujua kwao huyu dada kijijini, ilimlazimu huyu dada kumpeleka Mwanza kwa kaka yake.

Alipoulizwa na wazazi wake sababu ya kumpeleka mkwe mzungu kwa kaka yake badala ya nyumbani kwao ili nao wakapate ufahari kuwa binti yao ameolewa na mzungu, yule binti aliwaambia kuwa mme wake angeona ajabu kunya kwenye choo cha nje, tena choo cha shimo!

Ukipita mitaa ya Samora, Posta Mpya au Posta ya Zamani mjini Dar es Salaam, ni mitaa iliyo na wazungu sana, hasa wale wanaotaka kusafiri kwenda Zanzibar au kufanya ununuzi, kupata vibali mbalimbali za kuingia nchi nyingine, utaona vijana wakitanzania wakiwa wamejipanga wakiwakimbilia hawa wazungu na hata wale wasiojua kiingereza hujitahidi kwa namna yake ili mradi apate urafiki, amsindikize anakokwenda na hatimaye mkono uende kinywani.

Mwalimu wangu mzungu aliyenifundisha nikiwa katika kidato cha kwanza aliwahi kuniandikia baruapepe hivi majuzi katika barua hiyo moja ya vitu alivyoniambia ni kuwa kama kuna msaada wowote wa kipesa anaoweza kunipa katika shughuli ninayofanya nimjulishe.

Hivi sisi Waafrika hatuwezi kufanya mambo yetu mpaka msaada, hivi wazungu wanatupa mtazamo gani na wanatungalia kwa jicho gani? Ni lini tutawaonyesha kwa vitendo kuwa tunajiamini, tunaweza bila wao na kwamba wao sio Miungu watu walioletwa kuikomboa Afrika.

Wiki mbili kabla ya siku ya mtoto wa Afrika, nilifanikiwa kuhudhuria Zanzibar ilipokuwa ikifanyika kwenye moja ya hoteli ambapo tulikusanyika vijana wapatao 25 wa Kiafrika na wazungu idadi yao ilikuwa 20. Kama unavyojua Waafrika tunavyopenda kujitenga na kukaa peke yetu tukijadili mambo yetu.

Wahudumu wa ile hoteli wote waliwakimbilia wale wazungu na hata sisi kupata huduma nusu saa baadaye, wenzetu waliotoka Afrika ya Magharibi walianza kufoka na kufanya fujo wakisema sehemu zingine za bara hili Afrika bado inatawaliwa na wazungu!

Tunasikia katika masimulizi za Mabutu Seseseko kuwa maji yake ya kunywa yalikuwa yakitoka Ufaransa kwa ndege wakati mto Kongo ukisifika duniani kwa kuwa mto mkubwa na wenye maji masafi sana.

Charles Jonjo wa Kenya naye kuna kipindi tunaambiwa kuwa alikuwa akila vyakula vya makopo tu kutoka Ulaya na kwamba akidharau vyakula vya Kenya pamoja na kwamba vyakula vya asili ni vizuri kuliko vya makopo!

Dumnont katika kitabu chake cha Afrika Inakwenda Kombo aliwahi kutembela Afisa mmoja katika serikali ya Guinea Bissau, yule Afisa alipomwona kuwa ni mzungu alimletea juisi ya maembe ya makopo, Dumnont alikataa akamwomba kama ana maembe ya kawaida ampe au la, amtume mtu sokoni akamnunulie.

Yule Afisa alikataa kuwa sokoni hakuna maembe, kitabu kinaelezea kuwa alipokwenda mwenyewe sokoni alikuta maembe mengi na mengine yamekosa wanunuzi.

Na hivyo ndivyo hata ndugu zetu wengi Watanzania, wako tayari kununua maboga yaliyoletwa kutoka Afrika ya Kusini kwenye masoko kama shoprite, kuliko kunua maboga ya Kariakoo. Yuko tayari kununua mvinyo kutoka Italia na kuacha Tanganyika Wine ambayo ingemgharimu kiasi kidogo sana.

Siku ya maonyesho ya sabasaba Afisa Biashara mmoja aliyekuwa akisimamia banda lililokuwa na majani fulani yaliyotumika kutengeneza juisi, alikuwa akisisitiza kutumia vyakula vya asili na sio vya dukani, tulipowatembelea ofisini kwao kwa mahojiano zaidi baada ya maonyesho walitukaribisha kwa kutupatia juisi za Afrika ya Kusini iliyosindikwa kwenye makopo na sio juisi ile ya kwao inayotokana na majani ya mmea wa asili.

Dhana hii haijawatoka wengi, sio wasomi, wenye pesa, wanafunzi, wakulima, waliosoma Ulaya na hata viongozi wakubwa wa nchi zetu.

Dr. Martin Luther King Jr aliyepigania haki za watu weusi aliwahi kusema kuwa maisha ya mtu yanafikia kikomo siku ile anapoanza kukaa kimya juu ya mambo ya msingi yanahusu maisha yake.


0715 551455


Falsafa za Machiavelli


Tusikumbatie Falsafa za Machiavelli

Na Nyasigo Kornel

Katika moja ya imani ya mwanafalsafa mmoja wa Italia Machiavelli iliwataka viongozi wakuze sanaa ya udanganyifu kwa sababu aliamini kuwa watu werevu na wadanganyifu wakubwa ndio ambao wangeweza sanaa hatari ya utawala na siasa.

Mwanasayansi maarufu wa Ujerumani Albert Einstein alikataa kujiunga katika siasa za Ujerumani hata baada ya kuombwa kufanya hivyo, hatimaye aliwajibu akisema kuwa ‘Politics is more difficult than physics’ (Siasa ni ngumu zaidi kuliko fizikia).

Leo hii Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete anapoadhimisha mwaka mmoja wa kukaa madarakani kama rais, nadhani atakubaliana na Albert Einsten kuwa siasa ni ngumu kuliko fizikia. Uenda awe mbishi tu mdomoni.

Kuna msemo wa watu wa Ethiopia unaosema kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi mwanasiasa anaweza kujenga daraja hata pasipo na mto (During elections politician can build a bridge where there is no river).

Na ndivyo alivyofanya Rais wetu wakati wa kampeni yake, alitoa ahadi nyingi sana, alikula na watu wa chini mpaka wengi wakasema kuwa atakuwa kama sisi hata akipanda huko ikulu.

Nadhani ujasiri wa Rais wetu Jakaya ule wa maisha bora kwa kila mtanzania tena kwa kasi mpya, hari mpya na nguvu mpya sasa itakuwa imebadilika.

Wakati ule wa uchaguzi watu wa kima cha chini kama wamachinga walikuwa wakimwona mkombozi wao, leo hii wanamnunia, ndugu yao hawataki, wanamnung’unikia kweli.

Rais alikuwa ameahidi kutoa ajira milioni 1 kwa muda wote wa uongozi wake wa miaka 5 lakini tayari kwa mwaka mmoja tu ameshawapotezea watu wapatao milioni moja katika jiji la Dar es Salaam tu, hacha mikoa mingine. Hapa lazima akiri kuwa siasa ni ngumu.

Ripoti ya mwaka 1998 iliyotolewa na REPOA ilitoa idadi ya wamachinga jijini Dar es Salaam kufikia 850,000 hii ni asilimia 24 ya watu wote wanaoishi Dar es Salaam. Hawa wote amewajengea soko wapi, kama sio siasa?

Hata kama soko hilo lingelingana na uwanja wa Taifa unaojengwa kwa sasa ambalo linaweza kubeba watu laki sita tu, je ukiunganisha masoko yote ya Dar es Salaam inawatosha watu hawa laki nane na nusu?

Rais Kikwete na serikali yake nadhani watafurahi kuiona Dar es Salaam ina nyumba zenye kuta nzuri kama NewYork, Washington DC, London, Beijing na Tokyo hata kama watu wanaoishi kwenye huo mji ni ombaomba, kwa wanasiasa hayo ni maendelo ya miji.

Allen Prakash aliandika kitabu kiitwacho ‘Beautiful City of Beggars’ iliyohusu mji wenye ombaomba wengi sana kuliko miji yote duniani, mji wa Calcuta – India.

Katika kitabu hicho Allen anauliza ‘mji huu ni wa nani, ni ya majumba, magari au watu’? Sasa aje Tanzania awasemehe wamachinga.

Msomi mmoja wa Zimbabwe Prof. Nastroy Sizwe aliwahi kumwambia Rais Mugabe wa Zimbabwe wakati wa bomoaboma naye akiwa anataka Harare ipendeze kama miji ya Ulaya, Sizwe alimwambia kuwa ‘cities are not made, they evolve (miji haitengenezwi, yanatokea)’.

Miji hii yote ni ya watanzania na ni hao watanzania ndio wameanza kukusanya mitaji katika biashara hizo za kimachinga, taratibu watu wanakuwa wakifanana na miji yao kielimu, kijamii, kiuchumi na kimila.

Sasa hivi kupata hoteli Posta Mpya jijini Dar es salaam ya kula watu wa pato la kati hacha watu wa pato la chini ni kazi kweli. Kila hoteli utakayofika utakujikuta orodha ya vyakula inambagua mtu wa pato la kati, na watu wenye maisha ya aina fulani tu wakiwa wanapafanana.

Kwa sababu ya ukimya wa Mtanzania basi inakuwa ni kilio cha samaki, nani atawasemea.

Mwanaharakati Smith Adam aliwahi kutabiri miaka 90 iliyopita katika kitabu chake cha ‘Acquiring Wealth of the Nations’ akisema kuwa itafikia wakati maisha ya mwanadamu hayatakuwa na maana ila vitu kama viwanda, duka, magari, barabara na majumba ndiyo yatathaminiwa na serikali zetu.

Akatabiri kuwa na hapo ndipo mwanadamu atakuwa na chuki na serikali yake na hata kuwaza mapinduzi na vurugu. Na kwa hilo utajua kuwa siasa ni ngumu kuliko fizikia.

Wanabaki kujuta kuwa kumbe ile hari mpya ilikuwa ni ya kutoa ahadi hewa, kasi mpya ilikuwa ni ya kuwapa wanamtandao nafasi zote nyeti serikalini na nguvu mpya ya kujitangaza kwenye vyombo vya Habari, sasa ni muda wa kuwahoji kama kasi ya hiyo basi hilo analoliendesha ni sahihi au injini ni bovu.

Ni nafasi ya kujua kama kasi hii mpya ilikuwa ni ya kupeana madaraka miongoni mwa wafahidhina wa mtandao ambao wanaona sifa kujiita wanamtandao huku wengine wakishiriki kupunguza kasi mpya ambayo hatujui inakotupeleka.

Sekta ndogondogo ina mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa na ndio ina watanzania walio wengi, na kwa sababu ya matatizo ya umeme haziwezi kuzalisha kwa kiwango.

Siku chache tu Waziri Mkuu Edward Lowasa alinukuliwa na vyombo vya Habari akisema kuwa serikali ya awamu ya nne imerithi tatizo la umeme, akiwa na maana kuwa amelirithi kutoka kwa Serikali ya awamu ya tatu na pengine pia serikali ya awamu ya pili.

Huku ni kudanganya wananchi na kushindwa kuwajibika, ni kulikimbia tatizo kwani Waziri Mkuu Lowasa na hata Rais Jakaya Kikwete wote walikuwepo katika serikali ya awamu ya pili na awamu ya tatu, na pengine kuna mmoja kati ya hawa aliyefanya kazi katika wizara ya madini na nishati. Sasa wao wamelirithi kutoka kwa nani?

Dr. Martin Luther King Jr aliwahi kuwaambia ndugu zake Wamarekani weusi waliokuwa wakibaguliwa kwa rangi yao kuwa “Hatimaye mtu upimwa sio kwa pale aliposimama wakati wa raha na starehe, bali aliposimama wakati wa changamoto na matatizo”.

Mwanasiasa mmoja aitwaye Sir Winston Churchill alipoulizwa ujuzi ambao anatakiwa awe nayo mwanasiasa alisema kuwa ni uwezo wa kutabiri kitu ambacho kinaweza kutokea kesho, mwezi ujao na mwako ujao na kama isipotokea awe na uwezo wa kueleza sababu zilizoifanya isitokee.

Kitu kimoja ambacho mimi ninacho wasiwasi ni ukimya wa watanzania. Ukimya waliyonayo watanzania katika kutokuhoji juu ya haki zao za msingi na hata kushindwa kukataa yale yasiyopendeza kutekelezwa na serikali ni tabia ambayo inafaa tuiache.

Ingawa wanasiasa wanasema kuwa tabia ya kuwa kimya kutokuchokonoa kuwa ni cha kiustaarabu, mimi nasema ni ujinga, na pengine ndiyo inayotulimbikizia makosa mengi ndani ya nchi.

Ukitaka kumuudhi Mtanzania basi mlinganishe na Mkenya. Lakini ndio nchi tuliyonayo karibu sana, na kwa mfumo wake wa siasa ambao baadhi ya watu wanauita siasa za vurugu, mimi ninapenda kuita siasa za Kenya kama high-tech politics (Siasa zenye teknolojia ya juu) na zinaonyesha utawala bora.

Na pengine tumekuwa tukijisifia sisi watanzania kuwa tunajua siasa, sio kweli kabisa, siasa hizi za kuzibana midomo!

Mwanasiasa mashuhuri sana wa Kenya, Raila Odinga alihojiwa na BBC kuhusu hali ya vurugu za kisiasa Kenya na kama Kenya itaweza kufanikiwa kutulia vizuri kiuongozi kama ODM itaingia madarakani katika shirikisho la Afrika Mashariki na nchi yenye amani kama Tanzania.

Raila alijibu vizuri sana akisema kuwa kunakofuka moshi kuna uhai, na kimya kingi kina mshindo mkuu.

Siku chache tu kulifanyika uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki ambao uliambatana na mizengwe hata baadhi ya wabunge wa upinzani katika bunge la Tanzania kususia uchaguzi ule na hata kutoka nje.

Walichoambulia hawa wabunge wetu ni kejeli yaliyotolewa na Waziri mkuu Edward Lowasa akiwaambia kuwa wameidhalilisha Bunge, kuwa hawana hulka ya watanzania na zaidi wakaonekana ni watovu wa nidhamu.

Wabunge hawa badala ya kufuata mikondo ya sheria walirudi kulipigia kamati ya maadili magoti, wakaliomba msamaha na basi hadithi ikaishia pale.

Tofauti na wabunge wa Kenya, tena walikuwa ni wabunge watano tu, walichachamaa na hadi sasa sheria inachukua mkondo wake, je wabunge wetu wanalo la kujifunza kwa wabunge wa Kenya?

La hasha watasema sisi watanzania tuna tabia ya ustaarabu au wanasiasa wetu siku hizi wanaiita ‘hulka ya mtanzania’ maana yake ni tabia ya kukaa kimya bila kuuliza mambo, kama kondoo ambaye hata akichinjwa anakufa kistaarabu.

Katika barua aliyoandika Dr. Martin Luther King Jr. akiwa katika gereza la Birmingham iitwayo ‘Why We Can’t Just Wait (kwa nini hatuwezi kusubiri)’ anasema kuwa uhuru hautolewi kwa hiari na mshurutishi wako, bali anadaiwa kwa nguvu kutoka kwake.

Na hata Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliwahi kuwaambia wapinzani kuwa kwenye siasa usitegemee ‘fair play’ unakuwa mjeuri ‘no fair play in politics’. Ukishaitwa mpinzani basi wewe unajua namna ya kuinua sauti.

Kama wabunge wetu tunaotegemea wangetetea kondoo hawawezi kujitetea pale wanapotendewa kinyume na maadili, nao pia wamekuwa kondoo, sasa nani atusemee?

Ili serikali yoyote ile iweze kuamka ni lazima bunge liwe na wabunge wajeuri.

Katika historia ya Tanzania toka kipindi cha serikali ya awamu ya pili hili bunge la awamu ya nne ndilo bunge ambalo halijachangamka kabisa katika kuibua hoja za msingi. Hoja ya msingi zenye msingi wa kitaifa wanazipapasa juu juu tu.

Iko wapi bunge kama lile la wakati wa utawala wa Ali Hassan Mwinyi lililokuwa na kikundi cha G52 lililokuwa limechachamaa, likijiamini na kutikisa kwa hoja zenye mstakabali wa kitaifa?

Wako wapi wabunge kama akina Njelu Kasaka na shilingi zao walizokuwa wakitupa kusimamia hoja za msingi, au shida zimekwisha, au wamamziba mdomo, au naye ameungana na manyang’au?

Yuko wapi wabunge kama Mzindakaya aliyefanikiwa kumwondoa Idd Simba kwenye uwaziri kwa tuhuma za ufisadi? Au mafisadi wamekwisha au naye ameliunga mtandao wa mafisadi?

Viongozi wenyewe wamekithiri kwa vitendo vya rushwa tena zile kubwa kubwa katika zabuni ambapo bei halali ya kitu hakina uhalisia wa thamani yake.

Rais Goerge W. Bush wa Marekani baada ya kujikuta kuwa anatumia pesa za Marekani bila kutumia akili pale alipoivamia Afghanistani gazeti la NewYork Times ilimnukuu akijuta “Kuna maana gani kutumia kombora lenye thamani ya dola za Kimarekani milioni mbili kuvunja hema la watu wa Afghanistan lilo na thamani ya dola kumi?”

Mwalimu Nyerere alisema huwezi kuchanganya heshima na tamaa, na hii ndio kitu kinachotofautisha viongozi wetu wa kizazi hiki kipya na viongozi wale mahiri katika historia ya dunia hii kama Nyerere, Mahatma Gandhi na hata Mandela.

Pamoja na nchi za Magharibi kumnyima misaada kwa miaka sita, pamoja na kuwepo kwa vita vya Kagera, na uongozi kuwa bado mchanga, Mwalimu Nyerere aliweza kujenga nchi inayokuwa inajali raia wake wa kiwango chote cha maisha.

Katika vikwazo vyote hivi na uchanga wanchi, elimu ilipatikana bure toka shule ya msingi hadi chuo kikuu, kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika ilikuwa ni asilimia 90 hata Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika, huduma ya afya ilikuwa bure, tulikuwa na viwanda kama Mutex, Mwatex, Urafiki na mashiriki mengi yaliyokuwa na misingi ya kumwinua mkulima.

Leo hii ni kama tumelogwa, uongozi huu wa kizazi kipya wana vichwa vya bongo fleva! Pamoja na kuuza vyote alivyokusanya huyu mzee kwa miaka mingi, kuingiza wawekezaji, kuruhusu biashara huria, utajiuliza pesa hizi mbona hazileti huduma zile za msingi kwa raia kama kipindi cha utawala wa mwalimu?

Huwa najiuliza kuwa kwani yule Mwalimu Nyerere yeye pesa alikuwa akitoa wapi hata huduma zile nzuri zikapata kuwafikia watu bure?

Wiki tatu zilipita nilimwona Rais wa Urusi Vladimir Putin akihutubia kupitia katika televisheni ya nchi hiyo RT (Russia Today) katika siku yao ya mapinduzi ya nchi hiyo akiwaonya wanasiasa wake, alisema, “Mkitaka kujilimbikizia mali muache siasa mkafanye biashara, na yeyote anayetaka siasa ajifunze kutumia mshahara wake, kisha aje tushirikiane kufikiri pamoja namna ya kuupandisha huo mshahara.”

Siasa ni ngumu kama kiongozi ni mwongo na mhifadhi wa genge la ‘manyang’au).


0715 551455


Waalimu wa Sita


Waalimu wa Sita wasiwambwe msalabani

Na Nyasigo Kornel

Mshairi maarufu sana wa Uingereza aitwaye Shakespeare, katika tungo za mashairi yake aliwahi kuandika kuwa‘One way to get an education in a hurry is to drive a school bus’ (Njia mojawapo ya kupata elimu kwa haraka zaidi ni kuendesha basi la shule).

Hii ina maana kuwa kadri unavyokuwa karibu na watu wenye maarifa na ujuzi wowote basi uwezekano mkubwa wa kupata huo ujuzi kwa haraka ni mkubwa.

Siku sio nyingi waalimu waliopata mafunzo ya mwezi mmoja mara baada ya kuhitimu kidato cha sita wakijulikana kama ‘Waalimu wa Sita’ walikuwa wakipata changamoto katika vyombo vya Habari kuwa hawawezi kumudu kufanya kazi katika taaluma hiyo kwa muda huo mfupi wa mafunzo.

Imefikia hatua waalimu na wanafunzi katika mashule yao wanayofundisha wanawanyanyapaa na kuwapa majina mabaya sana kitaaluma wakiitwa ‘mabambucha’.

Wanasema nyani huchekana ngoko, hoja ni kwamba hawa waalimu hawana tofauti kubwa sana na wale waliopo kwani hata wale waliopo hawajathibisha utofauti wao kitaaluma.

Hiki kitendo tu inaonyesha kuwa walimu bado hawajui kuwa China walipokuwa na upungufu mkubwa wa waalimu katika miaka ya nyuma na idadi ya watu ilipoongezeka kuliko idadi ya waalimu, wanafunzi waliachishwa masomo ya sekondari bila mafunzo, na kisha waalimu wenzao waliwapa mafunzo wakiwa wanafundisha kwa vitendo.

Mwandishi maarufu wa makala ya elimu Hun Hwang wa shirika la Habari la China liitwalo Xinhua aliandika kuwa waalimu kama hawa walifanikiwa kuleta mapinduzi makubwa ya elimu katika historia ya China. Sababu ilikuwa ni kwamba walitaka kuthibitisha kuwa wao sio wa kiwango cha chini kama ilivyofikiriwa.

Hata katika miaka ya 1980, Indonesia ilitaka kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo na teknolojia, lakini waalimu waliokuwepo hawakuwa wamepata mafunzo sanifu katika nyanja hizi ambazo hapo awali hawakuwa wameipa kipaumbele. Walichoamua ni kuachisha masomo wanafunzi kutoka katika vyuo vya kilimo na ufundi kwenda mashuleni kufundisha.

Hadi hii leo, Indonesia inajivunia mapinduzi makubwa yaliyoletwa na vijana hawa na ni hapo ndipo hata wanafunzi wa shule za sekondari walipoweza hata kutoa mswada katika viwanda juu ya namna ya kutengeza pembejeo ya aina Fulani.

Utaratibu huu uitwa ‘crush program’ na inatumika pale ambapo serikali imeshindwa kuwianisha mipango ya muda mrefu na mahitaji ya jamii kama ongezeko la watu, hivyo inaamua kuzima moto kwa njia hii.

Badala ya kuzomea waalimu wazoefu kuwazomea waalimu hawa wa Sita wanatakiwa wawasaidie, huu ni upungufu mkubwa wa saikolojia ya mahusiano ambayo waalimu hawa ndio wataalamu wa masomo hayo.

Ukisoma katika kitabu cha ‘pedagogy of the Oppressed’ kilichoandikwa na msomi maarufu wa Brazil bwana Paulo Freire ambaye ameshiriki katika mapinduzi makubwa sana ya elimu nchini hapo, kinasema kuwa ‘teachers are not trained in the classroom but in the fields’ (waalimu hawaandaliwi madarasani bali wakiwa mazoezini).

Katika kitabu cha Prof. Ronald Dore kiitwacho ‘Diploma Disease’ (Magonjwa yatokanayo na kupata Stashahada) aliandika juu waalimu waliokuwa wakifikiri kuwa vyeti vyao vya diploma vingeweza kufanya kazi yenyewe mara baada ya kuhitimu bila jitihada za mwalimu kuwa mbunifu.

Prof Dore anasema kuwa siku hizi kazi ya ualimu unapatikana kwa maonyesho ya vyeti vya diploma na shahada. Anasema kuwa mashule yetu yamejaza waalimu wenye vyeti hivi vya diploma na shahada ambao wengine hawawezi hata kuongea mbele ya wanafunzi na wala sio hata wabunifu.

Aliuona ugonjwa huu wa diploma uliokuwa unawasumbua waalimu katika nchi nyingi alizofanya utafiti wake ikiwemo nchi ya jirani ya Kenya, Japani, Sri Lanka na Uingereza.

Huu ugonjwa wa diploma upo hata hapa Tanzania, tena umefanya hata hii taaluma ya ualimu kudharaulika. Na wanaofanya ualimu kuonekana kama ni taaluma ambayo kila mtu anaiweza ni hao hao waalimu wenyewe.

Miezi miwili iliyopita nilishiriki katika Warsha ya wiki moja iliyokutanisha baadhi ya waalimu wenye uzoefu wa kufundisha sayansi katika nchi za maziwa makuu mjini Nairobi, Kenya.

Ingawa nilishiriki kama mwandishi lakini mafunzo yangu ya ukufunzi wa masomo ya sayansi kwa vyuo vya ualimu ilinipa nafasi ya kujionea fikira potofu ambayo kama waalimu hawatayafuta basi hatutang’oka.

Moja ya mada iliyojadiliwa na waalimu hao wazoefu ilikuwa ni juu ya vikwazo wanazopata katika kufundisha masomo hayo ya sayansi mashuleni.

Mwalimu mmoja aliyewakilisha Tanzania akitokea Moshi alijibu kwa kusema kuwa hawana vitabu vya sayansi na zaidi aliendelea kuongea kwa jazba akisema kuwa tangu aanze kufundisha hajawi kuona aina yoyote ya kemikali na hata kifaa cha maabara, na zaidi ya yote mishahara ni midogo.

Waalimu wenzake kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walimpigia makofi huku wakiongezea kwa kusema, “sema yote mzee”.

Mwalimu wa kitanzania, tena aliyebora na aliyewakilisha wenzake anasema hajawahi kuona kemikali katika maabara! Je mchanga ni nini kama sio kemikali? Hajui kuwa ‘Calcium silicate’ ndio asilimia kubwa ya mchanga! Je maji ya limau na matunda hajui kuwa ni kemikali?

Mpaka serikali itumie mabilioni ya pesa kuagiza starch ambayo hata mwalimu angetumia ubunifu kidogo akaipata katika unga wa mihogo, sasa hivi starch inaagizwa kwa wingi hadi vyuo vikuu hawatengenezi starch vyao.

Dunia tuliyomo ni Kemikali, fizikia au baiolojia. Ukichukua pombe ya gongo ni kemikali, maji ni kemikali, nyongo ni kemikali, sabuni, maji ya miti, mate, mafuta, matope na mengine mengi.

Kumfundisha mtoto ili aelewe juu ya hewa ya oksijeni na kabondioksidi itakuhitaji kiberiti, mshumaa na mfuniko mkubwa tu kumthibitishia mwanafunzi kuwa kama hakuna hewa ya oksijeni basi mshumaa hauwaki, basi.

Huyu mwalimu aliyepigiwa makofi na walimu bora wenzake wa sayansi, hajawahi kuona kemikali, na hata hana wazo ya kutengeneza maabara ya sayansi inayojumuisha vitu vilivyopo katika mazingira yake. Lakini bado alipendekezwa na lile shirika kuwa ni mwalimu bora.

Na hili ni tatizo lililopo hata kwa waalimu wa chuo kikuu wanaowaandaa hawa waalimu. Leo hii mwalimu wa sayansi anaamini kuwa hawezi kufanya majaribio mpaka starch itoke China na Ufaransa. Hajui kuwa mihogo ni starch.

Leo hii katika Tanzania hii iliyojaa kompyuta na fotokopi karibia katika kila Mkoa wa Tanzania, mwalimu bado darasa lake linakoswa vitabu. Pale panapotokea upungufu wa vitabu vya rejea mwalimu wa kitanzania bado hawezi kutunga hata kitini na akapiga fotokopi kuziba pengo la vitabu.

Mwalimu wa darasa la kwanza anasubiri aletewe vitabu vya kujumlisha vilivyochapishwa na ‘Mture Book Publishers, Macmillan Aidan, E&D Publishers na Oxford University Press’. Aletewe vitabu vyenye silabi ‘a, e, i, o, u’ na vile vya namna ya kuandika mchorongo. Kwani mwalimu hawezi kutunga kitabu kimoja wakapiga fotokopi ikatosha darasa zima.

Mwalimu wa kitanzania hawezi kutunga hata kitabu ili kitumike shuleni, hata ya kujumlisha, za silabi, za kusoma na kuandika. Alafu leo waseme wanalo la kujivunia juu ya waalimu wa Sita! Wote wanafanana na kama utofauti upo ni mdogo sana unaoweza kuzibika kwa muda mfupi sana.

Ni waalimu wangapi wamejadiliana na Afisa Elimu wa Wilaya juu ya hilo wazo mbadala, na badala ya pesa za MMEM na MMES kununua vitabu vya makampuni makubwa waalimu wa aina hii wapewe ruzuku kama kazi zao ni nzuri.

Siku ya mwalimu duniani, mwalimu mmoja aliye na shahada ya sayansi aliongea katika runinga akisema kuwa shule yake aina hata kitabu kimoja cha fizikia. Mimi nafikiri huu ndio uvivu, uzembe na ujinga. Mtu wa chuo kikuu hauwezi kupambana na mazingira yako, na kutoa utatuzi wa tatizo hilo dogo.

Hivi kweli watoto wetu wasisome kwa kukoswa vitabu na mwalimu wa hilo somo ana shahada! Kama sio ugonjwa wa shahada au ugonjwa wa diploma ni nini sasa? Je mwalimu wa hivyo ni urithi kwa nchi hii kweli?

Wakati mwingine tumekuwa tukiilaumu serikali bure. Kama mtu amelipiwa na hiyo serikali yake na kusoma ili aisaidie nchi yake anakaa katika shule ambayo haina hata kitabu wala maabara, na anashindwa kuorodhesha aina ya mimea kisha akawahusisha wanafunzi wake, wakakusanya jamii mbalimbali ya mimea yenye misingi ya kisayansi na kisha wakatengeneza bustani ya botania.

Leo hii huyu mwalimu wa aina hii naye eti anamcheka mwalimu yule wa Sita kuwa hawajapata mafunzo ya kutosha. Mnawazidi nini?

Kuna lugha inayotumika katika ualimu inayoitwa ‘tabula rasa’ ikiwa na maana kuwa chombo tupu. Na mwalimu anashauriwa asimfanye mwanafunzi ‘tabula rasa’ kwa kumtafunia kila kitu na mwanafunzi kumeza tu.

Sasa hivi inavyoonekana ni kuwa waalimu ndio wamekuwa ‘tabula rasa’ na sio wanafunzi tena.

Plato mwanafalsafa aliyetoa nadharia nyingi sana katika elimu ay ualimu anaamini kuwa mitaala ya elimu ni vichocheo tu vya kuamsha elimu na maarifa na siyo viletavyo maarifa, hivyo anasisitiza majadiliano kama njia ya kuamsha maarifa nadni ya mwanafunzi.

Lakini mwanafalsafa mwenzake kama Aristotle anapingana naye kwa kuamini kuwa binadamu hazaliwi na maarifa bali huzaliwa na uweza wa kujua na kadri anavyokumbana na vitu vinavyoonekana ndivyo anavyopata maarifa.

Duche Smith aliwahi kuanzisha shule ya ualimu nchini Uingereza katika mtindo wa wanafalsafa hawa wawili yaani Plato na Aristotle, ambayo waalimu waliofuzu katika chuo chake walikuwa wakitafutwa kama keki duniani. Wale waalimu wa Duche hawakuhitaji hata vitabu na maabara. Wao walitaka wapewe mitaala tu. Walikuwa na msemo uliowasifia mbinu zao ikisema ‘just curriculum will show the means and ends’ (mitaala itaonyesha njia na matokeo yanayokusudiwa).

Hawakuwa waalimu wanaoogopa wakaguzi, hawakusimamiwa, walikuwa wakijiamini na kufanya kazi zao kwa hali ya juu sana. Walisaidiana na wanafunzi wao kuandaa vifaa vya kujifunzia hata notisi za mwalimu mwanafunzi aliweza kumletea hiki na kile akaongezea.

Dhana ya mwalimu kuibulia wanafunzi fikara pevu na kuwa na jamii ya watu wanaoweza kusimama na kudai haki zao hata pale wanapoonewa imekwisha potea.

Waalimu wamekuwa wakisubiri kusemewa hata katika mambo yanayohusu taaluma yao.
Huliza wakwambie kama hata wanapobadilisha mitaala kama wanashirikishwa!

Siku chache kabla ya ule mtaala wa Waziri wa awamu ya Tatu wa Wizara ya Elimu na Utamaduni Joseph Mungai kukataliwa, ni waalimu wasiofika 100 tu ndio waliokutana, na si ajabu hao waalimu waliokutana hawakuwa na uwezo yakinifu juu ya uchambuzi wa mitaala.

Sasa hivi utaona vitabu ambavyo wanafunzi wasoma, ni vile vitabu ambavyo haviibuhi fikira pevu kwa kizazi hiki tulichonacho. Ingawaje hatuna vile vitabu vingi vyenye kuibua ukombozi wa kifikra, lakini ijulikane kuwa wanasiasa wanataka watu wasifumbuke akili, wanataka tuwe madondocha ili wao na watoto wao watutawale bila kuzinduka.

Mwalimu Nyerere alichekesha akisema wanasiasa wanasema ujinga ni baraka.

Tazama, katika vitabu vya fasihi kwa shule za sekondari mwanafunzi anapewa kusoma kitabu kama ‘penzi kitovu cha uzembe au kile cha Hiba ya Wivu’ nyingi ni vitabu vyenye ladha ya mapenzi, na wanajua kuwa wanafunzi wetu wanapenda mambo ya mapenzi mapenzi, lakini ni nani aseme? Waalimu wako kimya, wanavichukua na kisha kuingia darasani na kuanza kuwacheulia watoto wetu.

Vitabu vyenye silika za ukombozi hawawezi kamwe kuwapatia wanafunzi wetu kama Almasi za Bandia kilichoandikwa na marehemu Prof. Seith Chachage, Makuadi wa soko huria na mengine kama hayo.

Mwanafunzi wa sekondari aliyesoma vitabu vya fasihi laini laini hizi za mapenzi huwezi kumlinganisha na yule anayesoma fasihi zenye falsafa na hamasa nzito kama vilivyoandikwa na mrusi Marxim Gorky ‘mama’ mrusi aliyetetea wafanyakazi wa viwandani hata kuleta mapinduzi ya viwanda.

Gazeti la NewYork Times liliandika kwa mandishi makuwa kabisa kuwa ‘teaching children to count is not as important as teaching them what counts’ (kumfundisha mtoto kuhesabu sio muhimu kama kumfundisha kuelewa yaliyobora.

Watu wengi walioshiriki katika ukombozi wa dunia hii waliibua vichocheo hizo wakiwa bado wapo mashuleni. Angalia historia ya Pan-African na hata maandamano yaliyofanywa na wanafunzi wa Soweto huku Afrika ya Kusini.

Mwalimu wa kitanzania hawezi kusema, hawezi kuuliza juu ya mtaala anaoletewa autumie, haulizi hata juu ya vitabu anavyotakiwa mwanafunzi aisome.

Ivan Illich, katika kitabu chake maarufu sana kwa wasomi wa elimu kiitwacho Celebration of Awareness, anawabeza waalimu ambao wakishapata vyeti wanalala, wanasherehekea kiwango chao cha uelewa, shahada zao na diploma hizo, hawajishughulishi kuibua mapinduzi ya kifikira katika taasisi za miongozo yao.

Ukitaka kujua ni kwa kiwango gani haya yametuletea madhara nenda mashuleni, utawakuta wanafunzi wa sekondari wamebeba majarida yale yenye michoro ya michafu kwenye jalada (Sexual arousal magazines). Huyu mwanafunzi, katika umri wa miaka ya sekondari tuseme 20, hataweza kuhoji mambo ya msingi yanayohitaji fikira nzito na huwezi kumlinganisha na mwanafunzi anayesoma vitabu vizuri.

Haitoshi tu kusema kuwa mwalimu ana diploma, shahada au amepata mafundisho ya mwezi mmoja. Tunataka tuwaone kwa matunda yao.

Hata yesu aliwaambia kuwa siku yaja ambapo kutakuwepo na manabii wengi hata wa uongo lakini alipoulizwa kuwa watawajuaje, aliwajibu wanafunzi wake kuwa mtawajua kwa matunda yao.

Simu: 0715 551455
Email: emmakornel@yahoo.com


Ibada za Kikoloni


Tunaendela kusali ibada za kikoloni

Na Nyasigo Kornel

WASOMI na watawala wetu wamekuwa wakimkejeli Chifu Magungo wa Usagara kwa kile kinachoitwa kutia sahini mkataba wa ulaghai wa kuwapa wakoloni ardhi kwa muda wa maika 999 chini ya mpelelezi Dk. Karl Peters.

Chifu Magungo analo la kujitetea, anaweza kusema kuwa hakuwa na elimu, taarifa na maharifa ya kutosha juu ya mikataba na dhana nzima ya ukoloni.

Hata katika miaka hii ambapo wasomi ndio wamekuwa watawala wan chi hii, bado tunaona mikataba kama hii ya Chifu Magungo zikiendesha.

Zimekuwa zikiingia ndani ya nchi kama makampuni, asasi au madhehebu za kididni.

Ukisoma kitabu cha ‘The Black Batch’ kilicholeta ugomvi na kuzua mjadala mkubwa mwishoni mwa karne iliyopita huku ikilaumiwa na wasomi wa nyakati hizo kuwa kimemtukana mwafrika, utaona jinsi gani wazungu wanavyotuona kama makatuni katika fikara zetu.

Kitabu hicho kinalaumiwa kwa kuandika siri na namna ya kumtawala Mwafika huku kikitumiwa na shirika la kijasusi la CIA kwa ajili ya kuwageuza wasomi wetu mabumbumbu wao.

Kitabu hicho kinasema, “Ni rahisi sana kumtawala msomi wa Kiafrika kuliko mwafrika asiye na kisoma, na kwa sababu mwafrika asiye na kisomo anamwamini nduyu yake aliyesoma, basi jitahada kubwa ya Mmarekani na wenzake iwe ni kuwanywesha kasumba.”

Sijui ni kwa nini wanapanafrikanizism walikichukia hiki kitabu na kukipigia kelele kuwa wamedharahuliwa wakati kilielezea ukweli kabisa.

Katika kitabu cha Prof Eduard Achermann kiitwacho ‘Cry Beloved Afrika’ au kwa kiswahili ‘Fumbuka Afrika’ anasema kuwa ilifikia hatua ndugu zetu, tena waliokuwa wapigania uhuru na demokrasia ya Afrika kama marehemu Mobutu Seseseko aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alikuwa hajui utaofauti kati ya akaunti yake na akaunti ya taifa.

Anasema hata rais Kerekou wa Benin alidhani Benki ya serikali ni mali yake binafsi.

Katika gazeti la wafanyabiashara iitwayo ‘Bilanz’ ambayo ilionyesha wapi mameneja wanalazima kuwapa rushwa wataalamu na kiasi gani ili waweze kupata mikataba, ramani hiyo iliyonyesha bara la Afrika.

Kitabu hicho kinasema kinanukuu wamisionari wa kizungu waliofikiri kuwa kwa kumsomesha mwafrika watawasaidia ndugu zao, wanasikitika kuwa kumbe walikosea, kwa maana walijikuta wakiwa wameunda wataalamu ambao waliwageukia ndugu zao na kujiunga na makampuni ya dunia ya kwanza na kutupora mali zetu.

Wiki hii tumemsikia Mh. Andrew Chenge akitutuliza Watanzania, akisema kuwa tusiwe kama Waingereza wanaouliza kuhusu rada tuliouziwa kwa bei ya kuruka, na hata kuwmeka Tonny Blair katika wakati mgumu.

Waingereza wameona kabisa kuwa sisi hatuna uwezo wa kuiuliza serikali zetu na kuiwajibisha juu ya mikataba mibovu wanayoifanya na makampuni ya nje.

Kinyume chake huku kwetu Bunge letu liko kimya, kwao hilo sio tatizo la kujadili. Bunge letu limekuwa kama vilabu vya mashoga‘gays clubs’ za Amerika ambapo ukifika unawakuta wanaume wasafi wakiwa wamevalia suti utadhani wanazungumzia biashara kubwa kubwa au hoja nzito za maendeleo, kumbe hamna lolote.

Bunge liko tayari kutumia siku kujadili kuhusu joho la Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano. Huyu akitaka iwe na picha ya hiki na mwingine akitaka iwe mpya ili mradi siku ipite.

Ilipofikia suala wananchi kutaka kujua juu ya ukweli kuhusu tuhuma za ufujaji wa pesa za wananchi kunua maghala ya ‘Quality Group’ Spika alisema hayo ni ya mahakama, wao wako bize wanajadili kuhusu joho la Spika.

Katika dunia ya leo ya Mtanzania, amejengewa akilini kuwa hawezi, tena kila anachokifanya akiwezi kufanikiwa. Na aliyetujengea mawazo hayo ni Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa.

Hili lilionekana katika mwenendo mzima wa uwekezaji, huku akibeza kwenye vyombo vya habari kuwa sisi hata tukiachiwa miradi hatuwezi.

Huyu Benjamin Mkapa ni mmoja wa matunda ya Pan-Afrikanism, wale watu waliokuwa wakitaka Waafrika wajikomboe, wajitambue, wajiamini na wawe tayari kulinda nchi zao.

Kumbe zile zilikuwa ni gia za Waafrika wasomi wa enzi hizo kunyemela madaraka mara baada ya mkoloni kutoka.

Kwani walipopata madaraka, katika baadhi ya wananchi walitamani mkoloni arudi, ndugu zao hawakujali kuwajengea mazingira ya uhuru kamili.

Mheshimiwa Idd Simba alipoongelea suala la ‘uzawa’ aliambiwa kuwa neno hilo halipo katika kamusi ya utandawazi.

Watu wenye akili kabisa walionekana kumpinga bungeni, kumbe wamejificha nyuma ya utandawazi ili watumie makampuni ya nje kutunyonya jasho la wananchi.

Mwalimu Nyerere alikuwa akiwaimbia hawa viongozi tulionao sasa hivi kuwa ‘pesa sio msingi wa maendeleo’. Inawezekana hawakuwa wanamwelewa kabisa, na pengine wengine walikuwa wakimwogopa kwa unafiki tu. Kwani hata baada ya kufa kwake watu wachache wanaoonekana kujua falsafa zake.

Leo hii utasikia wananchi wanashangilia kuona uhusiano mzuri wa Rais wa nchi yetu na Rais wa Marekani. Kwani hata kwenye vyombo vya Habari utaona katika kurasa za mbele zikiwa zimeandikwa ‘Bush akubali kuisaidia Tanzania’. Tunashangilia misaada na kuyakimbilia kumbe yanatuweka kuwa tegemezi.

Taratibu tutaanza kumchagua rais aliye na uwezo mkubwa wa kuombaomba. Lakini pesa hizi za misaada inatolewa katika maeneo ambayo hayatusidii.

Sasa hivi baadhi ya viongozi wetu hawana muda tena wa kutembelea wananchi, wanatafuta pesa kwa wahisani, wanafikiri nchi itaendelea kwa misaada. Maendeleo makubwa ya kwanza ni kubadili fikra za wananchi wako na kuwaambia kuwa wanaweza sio kuwatukana tena wazi kwenye vyombo vya habari kama alivyokuwa akifanya ndugu yetu mstaafu.

Juzi hapa nilipeleka makala yangu kwenye gazeti moja kubwa la kiingereza linalotoka kila siku, makala ilikuwa inazungumzia sera za Mwamerika, lakini haikutolewa.

Mhariri wa gazeti hilo alinitumia barua pepe na kuniambia kuwa hataki makala inayompinga George Bush na Rais Kikwete.

Mhariri huyo mwanamke alisema, “Rais wetu juzi alishikana mkono na Bush, sasa hivi Bush ni rafiki yetu, na tuko mbioni kufaidi misaada ya Amerika, hatutaki makala yanayowapinga kwa wakati kama huu ambapo tunaweza kutengeneza opportunities.”

Watanzania wengi bado tupo kama huyu mhariri. Hawa ndio wale ambao Plato, mwanafalsafa wa enzi za kati aliwaiita Doxa ‘watumwa wa mawazo’ ambao wanakodoa macho kwenye kivuli cha mwanga wakidhani ndio mwanga halisi.

Sasa nitumie makala hii kumjulisha kuwa maembe anayokupa mzungu sio ile unayohihitaji bali ni ile ilijaa hamira, na haishibishi.

Serikali za Ulaya na Amerika hao tunowashangilia kama Miungu watu, wanathamini na kujali ng’ombe wake mmoja kuliko maisha ya mwafrika mmoja.

Sasa hivi ripoti ya Benki ya Dunia inasema kuwa ng’ombe mmoja wa Ulaya analipwa ruzuku ya dola za Kimarekani 2 kwa siku na wanataka kuongeza zaidi, huku ng’ombe mmoja wa Japani anatolewa ruzuku ya dola za Kimarekani 4.

Hii ni zaidi ya mara mbili ya pato la Mwafrika ambao asilimia zaidi ya 40 uishi kwa chini ya dola moja kwa siku.

Mara nyingi hutoa mabilioni ya pesa sio kusaidia kilimo, kutafuta masoko, kujenga miundombinu vijijini na kutoa elimu bora.

Utaona pesa nyingi zinakuja ndani ya nchi kuzuia ukeketaji wa wanawake (Female Genital Mutilation - FGM), wakisema kuwa mwanamke hatendewi haki.

Kuna vikwazo vikubwa vinavyomkumba mwanamke na hasa wa vijijini kuliko swala hili la kukeketa. Inakadiriwa kuwa dola za Kimarekani trilioni 9 tu zikitumiwa vizuri, ingeweza kukwamua asimilia 80 ya wanawake kutoka katika umaskini uliokithiri.

Amerika inatumia kiasi hicho hicho cha dola trilioni 9 kwa mwaka kwa kununulia tiketi za kuingia kuangalia picha za sinema kila mwaka.

Katika Ripoti ya Dunia Kuratibu Misaada (Global Aid Monitoring Report) ilisema kuwa nchi za Afrika zimeshapata zaidi ya dola za Kimarekani trilioni moja kuzuia ukeketaji.

Kiasi hiki cha pesa ni mara nne ya misaada ya elimu kwa nchi za Afrika ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote.

Pesa nyingi zimetumika kuzuia suala la adhabu mashuleni. Wabunge wanatumika kutunga sheria hizi ambazo watu walio nyuma ya hizi sheria wamepewa mabilioni ya pesa.

Watoto haohao, ambao wazungu na asasi zao hizo wanaojifanya kuwahurumia kuwa wanachapwa viboko na adhabu mashuleni wana shida nyingi za muhimu kuliko viboko.

Utamkuta huyo mtoto hana sare za shule, hana uhakika wa kula chakula, hana madaftari na ana magonjwa yanayotibika ila huduma za afya ni mbovu.

Mtoto huyu huyu anayemhurumia anafika darasa la saba bila kuchapwa viboko anafaulu na hawezi kujilipia karo. Sasa kumtetea kwako kwenye viboko vimemsaidia nini?

Tunataka mtoto wa kitanzania aishi kama mtoto wa Swedeni na Norway, ambaye hachapwi viboko shuleni. Wakati mazingira ya mtoto wa Swedeni ni tofauti kabisa na huyu mtoto wa kitanzania.

Kuna haja gani kujifanya kuwa tunawahurumia watoto wetu kwa kutandikwa fimbo mbili nali hatuwahurumii kwa kulala njaa na kushindwa kuendelea na shule?

Hivi karibuni kuna makabila yalikataa kushurutishwa kuacha kukereketa wanawake na wakakataa.

Hata mimi, nawaunga mkono jamii hizo kwa kukataa. Hawaoni sababu ya wewe kumwonea huruma juu ya kile anachokipenda yeye na anakifanya kwa hiari, tena ikiambatanishwa na sherehe.

Leo hii eti atokee mtu kutoka mjini, yaani msomi, anajifanya anahuruma, wanaowaonea wanawake uchungu eti kwa sababu sehemu yao ya mwili umekatwa. Maskini jeuri… hawawaelewi.

Jamii inaongea taratibu (society speaks silent), kwa maana nyingine ni kuwa mbinu wanazotumia asasi hizi sio sahihi. Wanawapa wananchi wasichotaka kula na kuwanyima wanachokihitaji.

Katika ripoti ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere iliyojumuisha maoni ya wananchi juu ya kile wanachokihitaji kwanza ili waendelee. Wananchi waliorodhesha mabo yafuatayo kwa mtiririko; Elimu, kilimo, afya, usafiri, maji, utawala bora na ajira.

Wazungu hawatakupa pesa katika sekta hizi na hata wakikupa wanafadhili mradi usio endelevu. Na kibaya zaidi ni pale wasomi wetu ambao wangejitahidi kufanya hii miradi inufaishe taifa huwa upeo wao unakoma pale ambapo pesa za wahisani zinapoisha.


Email: emmakornel@yahoo.com
Cellular: 0715 551455