Saturday, January 13, 2007

Falsafa za Machiavelli


Tusikumbatie Falsafa za Machiavelli

Na Nyasigo Kornel

Katika moja ya imani ya mwanafalsafa mmoja wa Italia Machiavelli iliwataka viongozi wakuze sanaa ya udanganyifu kwa sababu aliamini kuwa watu werevu na wadanganyifu wakubwa ndio ambao wangeweza sanaa hatari ya utawala na siasa.

Mwanasayansi maarufu wa Ujerumani Albert Einstein alikataa kujiunga katika siasa za Ujerumani hata baada ya kuombwa kufanya hivyo, hatimaye aliwajibu akisema kuwa ‘Politics is more difficult than physics’ (Siasa ni ngumu zaidi kuliko fizikia).

Leo hii Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete anapoadhimisha mwaka mmoja wa kukaa madarakani kama rais, nadhani atakubaliana na Albert Einsten kuwa siasa ni ngumu kuliko fizikia. Uenda awe mbishi tu mdomoni.

Kuna msemo wa watu wa Ethiopia unaosema kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi mwanasiasa anaweza kujenga daraja hata pasipo na mto (During elections politician can build a bridge where there is no river).

Na ndivyo alivyofanya Rais wetu wakati wa kampeni yake, alitoa ahadi nyingi sana, alikula na watu wa chini mpaka wengi wakasema kuwa atakuwa kama sisi hata akipanda huko ikulu.

Nadhani ujasiri wa Rais wetu Jakaya ule wa maisha bora kwa kila mtanzania tena kwa kasi mpya, hari mpya na nguvu mpya sasa itakuwa imebadilika.

Wakati ule wa uchaguzi watu wa kima cha chini kama wamachinga walikuwa wakimwona mkombozi wao, leo hii wanamnunia, ndugu yao hawataki, wanamnung’unikia kweli.

Rais alikuwa ameahidi kutoa ajira milioni 1 kwa muda wote wa uongozi wake wa miaka 5 lakini tayari kwa mwaka mmoja tu ameshawapotezea watu wapatao milioni moja katika jiji la Dar es Salaam tu, hacha mikoa mingine. Hapa lazima akiri kuwa siasa ni ngumu.

Ripoti ya mwaka 1998 iliyotolewa na REPOA ilitoa idadi ya wamachinga jijini Dar es Salaam kufikia 850,000 hii ni asilimia 24 ya watu wote wanaoishi Dar es Salaam. Hawa wote amewajengea soko wapi, kama sio siasa?

Hata kama soko hilo lingelingana na uwanja wa Taifa unaojengwa kwa sasa ambalo linaweza kubeba watu laki sita tu, je ukiunganisha masoko yote ya Dar es Salaam inawatosha watu hawa laki nane na nusu?

Rais Kikwete na serikali yake nadhani watafurahi kuiona Dar es Salaam ina nyumba zenye kuta nzuri kama NewYork, Washington DC, London, Beijing na Tokyo hata kama watu wanaoishi kwenye huo mji ni ombaomba, kwa wanasiasa hayo ni maendelo ya miji.

Allen Prakash aliandika kitabu kiitwacho ‘Beautiful City of Beggars’ iliyohusu mji wenye ombaomba wengi sana kuliko miji yote duniani, mji wa Calcuta – India.

Katika kitabu hicho Allen anauliza ‘mji huu ni wa nani, ni ya majumba, magari au watu’? Sasa aje Tanzania awasemehe wamachinga.

Msomi mmoja wa Zimbabwe Prof. Nastroy Sizwe aliwahi kumwambia Rais Mugabe wa Zimbabwe wakati wa bomoaboma naye akiwa anataka Harare ipendeze kama miji ya Ulaya, Sizwe alimwambia kuwa ‘cities are not made, they evolve (miji haitengenezwi, yanatokea)’.

Miji hii yote ni ya watanzania na ni hao watanzania ndio wameanza kukusanya mitaji katika biashara hizo za kimachinga, taratibu watu wanakuwa wakifanana na miji yao kielimu, kijamii, kiuchumi na kimila.

Sasa hivi kupata hoteli Posta Mpya jijini Dar es salaam ya kula watu wa pato la kati hacha watu wa pato la chini ni kazi kweli. Kila hoteli utakayofika utakujikuta orodha ya vyakula inambagua mtu wa pato la kati, na watu wenye maisha ya aina fulani tu wakiwa wanapafanana.

Kwa sababu ya ukimya wa Mtanzania basi inakuwa ni kilio cha samaki, nani atawasemea.

Mwanaharakati Smith Adam aliwahi kutabiri miaka 90 iliyopita katika kitabu chake cha ‘Acquiring Wealth of the Nations’ akisema kuwa itafikia wakati maisha ya mwanadamu hayatakuwa na maana ila vitu kama viwanda, duka, magari, barabara na majumba ndiyo yatathaminiwa na serikali zetu.

Akatabiri kuwa na hapo ndipo mwanadamu atakuwa na chuki na serikali yake na hata kuwaza mapinduzi na vurugu. Na kwa hilo utajua kuwa siasa ni ngumu kuliko fizikia.

Wanabaki kujuta kuwa kumbe ile hari mpya ilikuwa ni ya kutoa ahadi hewa, kasi mpya ilikuwa ni ya kuwapa wanamtandao nafasi zote nyeti serikalini na nguvu mpya ya kujitangaza kwenye vyombo vya Habari, sasa ni muda wa kuwahoji kama kasi ya hiyo basi hilo analoliendesha ni sahihi au injini ni bovu.

Ni nafasi ya kujua kama kasi hii mpya ilikuwa ni ya kupeana madaraka miongoni mwa wafahidhina wa mtandao ambao wanaona sifa kujiita wanamtandao huku wengine wakishiriki kupunguza kasi mpya ambayo hatujui inakotupeleka.

Sekta ndogondogo ina mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa na ndio ina watanzania walio wengi, na kwa sababu ya matatizo ya umeme haziwezi kuzalisha kwa kiwango.

Siku chache tu Waziri Mkuu Edward Lowasa alinukuliwa na vyombo vya Habari akisema kuwa serikali ya awamu ya nne imerithi tatizo la umeme, akiwa na maana kuwa amelirithi kutoka kwa Serikali ya awamu ya tatu na pengine pia serikali ya awamu ya pili.

Huku ni kudanganya wananchi na kushindwa kuwajibika, ni kulikimbia tatizo kwani Waziri Mkuu Lowasa na hata Rais Jakaya Kikwete wote walikuwepo katika serikali ya awamu ya pili na awamu ya tatu, na pengine kuna mmoja kati ya hawa aliyefanya kazi katika wizara ya madini na nishati. Sasa wao wamelirithi kutoka kwa nani?

Dr. Martin Luther King Jr aliwahi kuwaambia ndugu zake Wamarekani weusi waliokuwa wakibaguliwa kwa rangi yao kuwa “Hatimaye mtu upimwa sio kwa pale aliposimama wakati wa raha na starehe, bali aliposimama wakati wa changamoto na matatizo”.

Mwanasiasa mmoja aitwaye Sir Winston Churchill alipoulizwa ujuzi ambao anatakiwa awe nayo mwanasiasa alisema kuwa ni uwezo wa kutabiri kitu ambacho kinaweza kutokea kesho, mwezi ujao na mwako ujao na kama isipotokea awe na uwezo wa kueleza sababu zilizoifanya isitokee.

Kitu kimoja ambacho mimi ninacho wasiwasi ni ukimya wa watanzania. Ukimya waliyonayo watanzania katika kutokuhoji juu ya haki zao za msingi na hata kushindwa kukataa yale yasiyopendeza kutekelezwa na serikali ni tabia ambayo inafaa tuiache.

Ingawa wanasiasa wanasema kuwa tabia ya kuwa kimya kutokuchokonoa kuwa ni cha kiustaarabu, mimi nasema ni ujinga, na pengine ndiyo inayotulimbikizia makosa mengi ndani ya nchi.

Ukitaka kumuudhi Mtanzania basi mlinganishe na Mkenya. Lakini ndio nchi tuliyonayo karibu sana, na kwa mfumo wake wa siasa ambao baadhi ya watu wanauita siasa za vurugu, mimi ninapenda kuita siasa za Kenya kama high-tech politics (Siasa zenye teknolojia ya juu) na zinaonyesha utawala bora.

Na pengine tumekuwa tukijisifia sisi watanzania kuwa tunajua siasa, sio kweli kabisa, siasa hizi za kuzibana midomo!

Mwanasiasa mashuhuri sana wa Kenya, Raila Odinga alihojiwa na BBC kuhusu hali ya vurugu za kisiasa Kenya na kama Kenya itaweza kufanikiwa kutulia vizuri kiuongozi kama ODM itaingia madarakani katika shirikisho la Afrika Mashariki na nchi yenye amani kama Tanzania.

Raila alijibu vizuri sana akisema kuwa kunakofuka moshi kuna uhai, na kimya kingi kina mshindo mkuu.

Siku chache tu kulifanyika uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki ambao uliambatana na mizengwe hata baadhi ya wabunge wa upinzani katika bunge la Tanzania kususia uchaguzi ule na hata kutoka nje.

Walichoambulia hawa wabunge wetu ni kejeli yaliyotolewa na Waziri mkuu Edward Lowasa akiwaambia kuwa wameidhalilisha Bunge, kuwa hawana hulka ya watanzania na zaidi wakaonekana ni watovu wa nidhamu.

Wabunge hawa badala ya kufuata mikondo ya sheria walirudi kulipigia kamati ya maadili magoti, wakaliomba msamaha na basi hadithi ikaishia pale.

Tofauti na wabunge wa Kenya, tena walikuwa ni wabunge watano tu, walichachamaa na hadi sasa sheria inachukua mkondo wake, je wabunge wetu wanalo la kujifunza kwa wabunge wa Kenya?

La hasha watasema sisi watanzania tuna tabia ya ustaarabu au wanasiasa wetu siku hizi wanaiita ‘hulka ya mtanzania’ maana yake ni tabia ya kukaa kimya bila kuuliza mambo, kama kondoo ambaye hata akichinjwa anakufa kistaarabu.

Katika barua aliyoandika Dr. Martin Luther King Jr. akiwa katika gereza la Birmingham iitwayo ‘Why We Can’t Just Wait (kwa nini hatuwezi kusubiri)’ anasema kuwa uhuru hautolewi kwa hiari na mshurutishi wako, bali anadaiwa kwa nguvu kutoka kwake.

Na hata Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliwahi kuwaambia wapinzani kuwa kwenye siasa usitegemee ‘fair play’ unakuwa mjeuri ‘no fair play in politics’. Ukishaitwa mpinzani basi wewe unajua namna ya kuinua sauti.

Kama wabunge wetu tunaotegemea wangetetea kondoo hawawezi kujitetea pale wanapotendewa kinyume na maadili, nao pia wamekuwa kondoo, sasa nani atusemee?

Ili serikali yoyote ile iweze kuamka ni lazima bunge liwe na wabunge wajeuri.

Katika historia ya Tanzania toka kipindi cha serikali ya awamu ya pili hili bunge la awamu ya nne ndilo bunge ambalo halijachangamka kabisa katika kuibua hoja za msingi. Hoja ya msingi zenye msingi wa kitaifa wanazipapasa juu juu tu.

Iko wapi bunge kama lile la wakati wa utawala wa Ali Hassan Mwinyi lililokuwa na kikundi cha G52 lililokuwa limechachamaa, likijiamini na kutikisa kwa hoja zenye mstakabali wa kitaifa?

Wako wapi wabunge kama akina Njelu Kasaka na shilingi zao walizokuwa wakitupa kusimamia hoja za msingi, au shida zimekwisha, au wamamziba mdomo, au naye ameungana na manyang’au?

Yuko wapi wabunge kama Mzindakaya aliyefanikiwa kumwondoa Idd Simba kwenye uwaziri kwa tuhuma za ufisadi? Au mafisadi wamekwisha au naye ameliunga mtandao wa mafisadi?

Viongozi wenyewe wamekithiri kwa vitendo vya rushwa tena zile kubwa kubwa katika zabuni ambapo bei halali ya kitu hakina uhalisia wa thamani yake.

Rais Goerge W. Bush wa Marekani baada ya kujikuta kuwa anatumia pesa za Marekani bila kutumia akili pale alipoivamia Afghanistani gazeti la NewYork Times ilimnukuu akijuta “Kuna maana gani kutumia kombora lenye thamani ya dola za Kimarekani milioni mbili kuvunja hema la watu wa Afghanistan lilo na thamani ya dola kumi?”

Mwalimu Nyerere alisema huwezi kuchanganya heshima na tamaa, na hii ndio kitu kinachotofautisha viongozi wetu wa kizazi hiki kipya na viongozi wale mahiri katika historia ya dunia hii kama Nyerere, Mahatma Gandhi na hata Mandela.

Pamoja na nchi za Magharibi kumnyima misaada kwa miaka sita, pamoja na kuwepo kwa vita vya Kagera, na uongozi kuwa bado mchanga, Mwalimu Nyerere aliweza kujenga nchi inayokuwa inajali raia wake wa kiwango chote cha maisha.

Katika vikwazo vyote hivi na uchanga wanchi, elimu ilipatikana bure toka shule ya msingi hadi chuo kikuu, kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika ilikuwa ni asilimia 90 hata Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika, huduma ya afya ilikuwa bure, tulikuwa na viwanda kama Mutex, Mwatex, Urafiki na mashiriki mengi yaliyokuwa na misingi ya kumwinua mkulima.

Leo hii ni kama tumelogwa, uongozi huu wa kizazi kipya wana vichwa vya bongo fleva! Pamoja na kuuza vyote alivyokusanya huyu mzee kwa miaka mingi, kuingiza wawekezaji, kuruhusu biashara huria, utajiuliza pesa hizi mbona hazileti huduma zile za msingi kwa raia kama kipindi cha utawala wa mwalimu?

Huwa najiuliza kuwa kwani yule Mwalimu Nyerere yeye pesa alikuwa akitoa wapi hata huduma zile nzuri zikapata kuwafikia watu bure?

Wiki tatu zilipita nilimwona Rais wa Urusi Vladimir Putin akihutubia kupitia katika televisheni ya nchi hiyo RT (Russia Today) katika siku yao ya mapinduzi ya nchi hiyo akiwaonya wanasiasa wake, alisema, “Mkitaka kujilimbikizia mali muache siasa mkafanye biashara, na yeyote anayetaka siasa ajifunze kutumia mshahara wake, kisha aje tushirikiane kufikiri pamoja namna ya kuupandisha huo mshahara.”

Siasa ni ngumu kama kiongozi ni mwongo na mhifadhi wa genge la ‘manyang’au).


0715 551455


No comments: