Saturday, January 13, 2007

Kilimo


Kilimo: Mdau muhimu wa matumbo anayesahaulika

Na Nyasigo Kornel


Aliyekuwa Waziri Mkuu wa India Hayati Mahatma Gandhi aliwahi kusema kuwa kuna watu katika dunia hii walio na njaa ya chakula kiasi kwamba hawawezi kuuona uhalisia wa Mungu wao katika maisha yao isipokuwa katika maumbo ya chakula tu (There are people in the world so hungry, that God cannot appear to them except in the form of bread).

Kauli hii ilileta changamoto kubwa hadi ombaomba wakaondolewa kwenye mahekalu ya wahindhu katika mji wa Calcuta, mji huo unaongoza kwa ombaomba wengi duniani waliokuwa wakilala tu bila kufanya kazi na kusali kwenye mahekali ya wahindhu.

Lakini hata pale walipopelekwa kulima vijijini, hali zao hazikuweza kubadilika kwa maana mbinu za kilimo na masoko hazikuwawezesha kuzalisha haraka hivyo wengi wao walirudi kuombaomba mijini.

India washukuru mapinduzi yaliyofanyika kuiweka Asia kuwa kijani dhidi ya ujangwa (Green Revolution) iliyotokea Asia miaka 40 iliyopita vinginevyo wangekuwa pabaya katika sekta ya kilimo kama ilivyo Tanzania iliyosahau wakulima ambao ni wadau muhimu wa maendeleo na kuwakumbuka wakati wa uchaguzi tu.

Wakati wa kikao cha Bunge lililopita, Mbunge wa viti maalumu, Mhonga Ruhwanya (CHADEMA), alitaka kujua kama serikali haioni umuhimu wa kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa njia mbalimbali kama redio, televisheni na magazeti pamoja na kutoa semina ya kilimo kwa wakulima kwa kutumia wataalamu wa kilimo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Christopher Chiza, alisema mbinu ambazo zimekuwa zikitumiwa na Wizara yake ni pamoja na kutengeneza gazeti la kisasa, vipeperushi, mabango na vijitabu vyenye ujumbe mbalimbali za kilimo bora na kuzisambaza kwa wakulima.

Mtu makini hawezi kukubaliana na Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Christopher Chiza, kwa msingi kuwa Serikali imekuwa ikijiweka mbali sana na wakulima kiasi kwamba mawasiliano hufanyika kwa vyombo vya Habari kama vipeperushi, vijitabu na mabango.

Tofauti na wanavyowatendea wakulima, ukienda kuandika Habari zao za semina utawaona viongozi wako tayari kukaa pamoja wakila na kunywa na mashirika yenye uwezo wa kuandaa semina zenye pesa, kwenye mahoteli kama MovenPick, Kilimanjaro, New Afrikan na mengine ya Bagamoyo.

Lakini hawako tayari kukutana na mkulima ispokuwa kwa njia ya vyombo vya Habari, kwani wakulima hawawezi kuwapatia posho za siku za vikao vyao.

Wakulima watapata wapi pesa za kuwalipa kila siku za semina? Je wakulima wataweza kufanya vikao vyao na kuvutia viongozi wetu kama wafanyavyo umoja wa wenye viwanda, mabenki, Asasi kubwa za nje na mashirika mengine yenye pesa.

Wakulima watawasiliana nao kwa njia ya magazeti, vipeperushi, mabango na vijitabu! Wasomi wa mjini wanaomiliki shirikisho mbalimbali na mashirika yenye pesa watakaa nao meza moja na kujadili juu ya matatizo yao na kisha ufikia muafaka na makubaliano ya mambo yanaathiri kazi zao na kweli wanasikilizwa.

Leo hii nina uhakika mkulima hatapenda kusoma vitabu bali atapenda kufanya kilimo cha vitendo, unampelekea mkulima bango, leo hii bango moja utakuwa umeandika nini cha kumwelekeza mtu juu ya kilimo cha kisasa na kufanya mapinduzi ya kilimo!

Waziri wa Kilimo na Chakula aliwahi kutamka kuwa Tanzania ina upungufu wa maofisa ugani 8,200 na waliopo ni 3,800 ambao hawatoshelezi.

Mwaka juzi vijana zaidi ya 60 waliomaliza Chuo cha Kilimo cha Sokoine wakiwa na shahada zinazoendana na taaluma ya kilimo waliajiriwa kuwa maafisa mikopo na National Microfinance Bank na wakasambazwa wilayani na mikoani.

Huku nchi ikikosa uelekeo katika kilimo cha kisasa hawa vijana hawatumiki vilivyo hata kama wangeamua kwenda kufanya kazi katika taaluma hiyo ya kilimo.

Mwandishi wa kitabu cha ‘Afrika Inakwenda Kombo’ Prof. Dumnont hakukosea aliposema kuwa baada tu ya mwafrika kupata elimu aliiona shughuli ya kilimo kama laana kubwa ya kuepukana nayo kwa namna yoyote.

Mwandishi huyo anasema kuwa hata sasa ni rahisi msomi wa kiafrika kumpelekea baba na mama yake sanduku nzima ya vitenge na suti lakini sio pembejeo za kilimo.

Katika moja ya safari ya kufanya tathmini ya kilimo na shirika la nje ya nchi ya Micro Agriculture Neighbours- MAN kama mwandishi tulifika katika ofisi ya Afisa Ugani Wilayani zaidi ya mara saba kwa siku tatu, hakupatikana, tukadhani kuwa yuko mashambani ambapo ingelikuwa ni vizuri.

Lakini moja wa makarani wa Wilaya aliamua kuongea akisema, “wale hawana kazi, atakuwepo tu kwake au niwalekeze dukani kwake mnaweza kumkuta.”

Na wale wazungu wageni walishangaa kusikia Afisa hana kazi za kutosha ofisini na hivyo anafanya biashara zake!

Sikuweza kumlaumu huyu Afisa kwa maana hata wakubwa wake hawajali wakulima.

Katika msafara huo uliojumuhisha baadhi ya viongozi wa Wilaya, nilishangaa kuona kuwa maafisa ugani kutoka Kenya ndio walikuwa wakiwaeleza wananchi namna ya kubebesha matunda ili kupata mazao bora kwa muda mfupi (artificial grafting).

Micro Agriculture Neighbours walifanikiwa kuwapatia wakulima wa pale mpakani mbegu za bure za mazao ya muda mfupi zinazoweza kuhimili ukame na kutoa mazao mengi.

Kwa ripoti niliyotumiwa wiki iliyopita kwa njia ya barua pepe na watu wa Micro Agriculture Neighbours ni kuwa wanakijiji wamekuwa waking’ang’ania zile mbegu na hata kuziiba mashambani wakati wa usiku.

Na waliporudi katika vile vijiji walipokelewa na kikundi kubwa sana cha wakulima waliohitaji kugawiwa zile mbegu na kupota elimu ya kubebesha mazao.

Hii ni kielelezo kuwa Maafisa ugani wa kwetu hawana mbinu mpya inayoweza kumvutia mkulima na ndio maana wakulima wetu hawawatumii huku vijijini.

Wengi wa maafisa ugani wetu wamekuwa wakifundisha mbinu za kilimo cha mistari ambapo uzoefu unaonyesha kuwa wakulima wamekuwa wakiikejeli kwa maana haitibu matatizo yao ya kilimo katika nchi za kitropiki.

Kama ulifuatilia mkutano wa Bunge lililopita Mbunge wa CUF kwa viti maalumu Magdalena Sakaya naye alisema kuwa uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya maafisa ugani wamejisahau na hawatekelezi majukumu yao.
Ukiona wingi wa maji katika Ziwa Victoria, utamwonea huruma mwananchi ambaye mihogo yake iliyopandwa hatua ishirini tu kutoka katika hilo ziwa ikiwa inaungua kwa kukosa maji.
Wakati huo windmill mbili kubwa inayoweza kutengenezwa na mtanzania, tena wale wa viwanda vidogovidogo vya kuchomelea kwa kutumia gesi inaweza ikaokoa maisha ya kilimo kwa kijiji kimoja lenye eneo la hekari za mraba 400.
Na windmill za aina hii pamoja na tenki la kuhifadhia maji na mipira ya kupitisha maji katika eneo kama hili haifiki hata zaidi ya shilingi milioni 20 kama hakuna rushwa na ufisadi.
Njia hii ya kumboreshea mkulima mazingira ya kilimo na kutatua tatizo la ukame linamwezesha mkulima kulima kwa mwaka mzima bila kujali kipindi cha mvua huku akibadilisha kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Kiongozi mmoja wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa moja ya jimbo jipya katika mkoa Mara alilalamikiwa kwa kutumia pesa nyingi zaidi ya milioni 300 katika uchaguzi wa Ubunge 2005.
Ingawa hakuna aliyejua alikotoa zile pesa alizokuwa akigawiwa kwa watu mbalimbali ili aweze kupata kura za ubunge, lakini hoja kubwa ni kuwa hizi pesa zilitosha kuleta changamoto katika mapinduzi ya kilimo kwa wananchi wa jimbo lile na pengine angechaguliwa bila hata kutoa rushwa.
Lakini mwanasiasa kama huyu hutumia milioni 300 kutoa rushwa ili apate kura wakati kiasi hiki hiki cha pesa kingeweza kujenga mifumo ya umwagialiaji wa njia hii kama kumi katika vijiji 7 kando ya ziwa Victoria na vikaendesha kilimo cha umwagiliaji.
Na sio hivyo tu, mabilioni ya pesa hutumika kununulia vitu visivyo na thamani kwa Mtanzania nail hiyo pesa ingeweza kuleta mapinduzi makubwa kwenye kilimo.
Ndio maana Ronald Regan aliyekuwa Rais wa Marekani aliwahi kusema kuwa serikali ni sawa na mtoto mdogo, ina utumbo wenye hamu sana ambao kwa upande mmoja unahitaji kula na kwa upande mwingine hautaki kuwawajibikia wengine (Government is like a baby. An alimentary canal with a big appetite at one end and no sense of responsibility at the other).
Sasa hivi Serikali ipo tayari kuonyesha kujali watu wakati wa njaa, na hata kuchangisha mashirika, watu mbalimbali na wafanyabiashara kuwagawia watu chakula, lakini serikali hiyo hiyo uanza usingizi mnene njaa inapokwisha.
Hii imefanya nchi kuwa ombaomba wa chakula na hakuna aibu kubwa kama ile wakati viongozi wetu wanapata sifa kubwa kimataifa na hata wengine kuchaguliwa kama viongozi wa kamati za kimataifa!
Katika mila za jamii nyingi za Kiafrika moja ya adha kubwa anayoipata mwanaume ni kushindwa kulisha familia yake na kuanza kuombaomba chakula kwa jirani.
Siku sio nyingi nilipata nafasi ya kuongea na Wamexico wanaomiliki shule ya sekondari ya Masonga katika kijiji kimoja kidogo cha Masonga kilichopo katika inayotegewa kuwa Wilaya mpya ya Rorya.

Hawa Wamexico wanatumia mfumo huu wa windmill kwa kuendesha kilimo cha umwagiliaji. Hata wao wanasema kuwa wametumia pesa kidogo chini ya makadiro niliyoweka pale juu maana

Eneo lile la Masonga lilikuwa limekwisha kuwa jangwa, watu walikata miti yote na ukabaki uwanja ambao uliweza kumwona mtu aliyesimama umbali mrefu sana, lakini nenda upaone leo, pamekuwa msitu tena pori kama vile hakuna shughuli za kibinadamu zilizowahi kufanyika pale.

Wanatumia njia hii ya windmill kusukuma maji hadi kwenye tenki la kutunza maji (water reservoir) na kisha kuisambaza sehemu mbalimbali kwa njia ya mifereji na mabomba ya kawaida.

Hivi leo wale wazungu wanasafirisha nje ya nchi asali, matunda kama maboga, tikiti maji, machungwa na aina nyingine ambazo hata sijawahi kuziona.

Pamoja na wananchi wale kuwa na huduma zile za kilimo cha umwagiliaji karibu, niligundua kuwa walikuwa hawalimi bali wengi walikuwa wakijihusisha na uvuvi wa samaki, hivyo wakati wazungu hawa wakipata pesa za kigeni kwenye kilimo, watu wa Masonga walikuwa wakikumbwa na njaa kila mwaka.
Leo hii pesa kidogo sana ingewezesha kilimo cha umwagiliaji kwa ziwa Victoria na Tanganyika tu, basi tungeweza kulisha nchi yetu na nchi nyingi sana za kusini mwa jangwa la Sahara.
Misri, nchi iliyojangwa inatushinda, hawana njaa, na kwa miaka 20 sasa hawajaomba misaada ya chakula kwa nchi yoyote duniani.
Katika tahariri la gazeti la Ulaya liitwalo The Private Eye linalohaririwa na Jonathan Wright limeandika juu ya mradi wa Toshka uliopo katika Aswan High Dam.
Mhariri wa The private eye amenukuliwa akisema kuwa pamoja na Misri kuwa jangwa lakini imefanikiwa kuibadilisha uso wa jangwa na kuwa kijani kama nchi za kitropiki na imefanikiwa kutosheleza soko la Ulaya kwa nyanya na viazi.
Juzi juzi Televisheni ya Al-Gezira ilinukuliwa ikitangaza kuwa mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia Alwaleed bin Talal atahamisha kiasi kikubwa cha ndege zake kuchukua matunda ya Misri, nchi ya Jangwa na kupeleka kuuza katika masoko ya Ulaya.
Ingawa mradi wa Answan High Dam ilijengwa katika miaka ya 1960 lakini ilianza mapema sana na hata Herode aliandika miaka 2000 iliyopita kuwa Misri sio kitu kama sio zawadi ya mto Nile, na asilimia 97 ya watu wa nchi hiyo huishi katika bonde la huo mto upatao asilimia 2.5 ya ukubwa wa hiyo nchi.
Na sio hapo tu nchi hizi za Mesopotamia ambapo ukiangalia jiografia yake ni nusu jangwa au jangwa kabisa zimejitahidi katika kilimo cha umwagiliaji, kwa mfano umwagiliaji unaofanyika katika bonde la San Joaquin, Rio Grande, Indus, Nile, Murray-Darling, Jordan na Tigris-Euphrates.
Katika waraka wa Papa Yohani Paulo II iitwayo tumaini jipya (Centesimus Annus) aliwaambia wanasiasa waache dhana kuwa kila tatizo kubwa la kijamii huitaji pesa nyingi sana kutatuliwa na alisema hayo kwa sababu viongozi wengi hutumia pesa ovyoovyo wakijificha nyuma ya matatizo ya kijamii.

Leo hii hakuna anayeongelea tahadhari ya njaa, hakuna anayechukua tahadhari ya ukame, hakuna anayemwangalia mkulima wa kijijini huko.

Na hata akishalima hakuna anayejali kama amepata soko au la, wanajitihidi ndugu zetu kwa hali na mali lakini ikifika wakati wa uchaguzi baadhi ya wagombea wenye pesa humimina pesa nyingi ambazo wangeweza kukaa pamoja chini wangelipanga mikakati endelevu.

Wakulima wa mihogo leo hii wameiacha lile zao likawa kama zao la chakula na kama wakitokea wanunuzi wa lile zao hulinunua kwa bei ndogo sana. Mkulima hujipatia pesa kidogo pale anapotengeneza pombe haramu ya gongo.

Hivyo ujenzi wa viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza pombe za moshi (small distilleries industries) kwa kutumia mihogo ya mtanzania ingeweza kumpatia soko kubwa mkulima huyu.

Indonesia hulima mihogo lakini hawaitumii kwa chakula, wanachokifanya Indonesia ni kuwauzia Warusi mihogo ile na ndio sehemu kubwa ya dry-gin tunazouziwa hapa ikiwa na majina mbalimbali ya kibiashara.

Na wanapolima mihogo wanaichanganya kwenye mashamba ya zao la mpira na hivyo umpatia pesa haraka hata mara mbili kabla hata la zao la mpira kukomaa zikipandikizwa kwa pamoja.

Hivyo kwa Indonesia zao la mihogo ni zao la biashara tena lenye pesa sana, na kwa mtanzania zao la mihogo ni zao la chakula.

Leo hii wakazi wa Wilaya ya Tarime wanaolima mihogo wanakunywa sana pombe za shilingi mia tatu za kwenye viroba kutoka katika viwanda vya Kisumu-Kenya.

Mwaka huu nilipofika Wilaya ya Liwale- Lindi wananchi wa pale wanaidharau mihogo na kuona kuwa wale wanaokula mihogo ni watu wa maisha ya chini sana na inapaswa kuliwa pale tu unapokosa unga wa mahindi na nafaka zingine.

Suala la kilimo haiishii tu kusema ukulima wa kisasa, kwa maana kama soko nzuri haipo basi wakulima watakata tamaa na wengi wa vijana watalazimika kukimbilia mijini kutafuta kazi za haraka zinazoweza kuwapa riziki haraka.

Sasa hivi zao la korosho limekuwa tena laana kwa wakazi wa kusini badala ya kuwa neema kwao kwa kukosa soko la zao hilo.

Kilimo cha katani sio mada tena ya kuongelea Tanzania wakati nchi kama Pakistani zao hili uingiza asilimia 0.1 ya pato la Tiafa hilo.

Soko linalotafutwa nje ya nchi ni ya nini? Ni la zao la Korosho au malighafi inayotokana na korosho? Au ni soko la katani au malighafi inayotokana na korosho?

Kama bado tunafikiri kuwa utauza hata asali nchi za nje kama asali na sio kama gem, basi kuna ugomvi mkubwa sana kwa viongozi watakaoiongoza nchi hii iliyolimbikiziwa matatizo ya wakulima katika miaka 10 ijayo.

Hata viwanda vya samaki tungependa kuona wakisafirisha nje ya nchi nyama ya makopo iliyo na trademark ya Tanzania na sio minofu, minofu haina trademark ya Tanzania na hivyo upunguza nukuu inayoleta urari wa kibiashara kati ya Tanzania na nchi za nje.

Sasa hivi wale wote wanaowekeza hapa utakuta viwanda vya muhimu vipo kwao huko Afrika ya Kusini au Ulaya na vile vya kudokolea mali zetu ndio ziko huku.

MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRIKA

0715 551455



No comments: