Saturday, January 20, 2007

Karugendo Usitetee Vijimungu vya Akili


Karugendo Usitetee Vijimungu vya Akili

Na Nyasigo Kornel

Mwanafalsa maarufu sana Fransis Bacon aliwahi kukusanya manung’uniko dhidi ya wasomi katika maandiko yake ya ‘distempers of learning’ yaani magonjwa ya elimu na vijimungu vya akili ‘idols of mind’ yakilaumu wasomi kwa magonjwa waliyoambukiza watu ya kupotosha elimu na maarifa.

Mahali popote pale ambapo binadamu mwenye akili timamu anaishi na siyo mfu, hapakosi mapambano ya hoja. Lakini pamoja na hayo yote, hakuna kipindi ambacho Tanzania katika uhai wake inahitaji uchambuzi wa kina kama kipindi hiki cha mpito wa kifikra.

Mwandishi maarufu sana wa vitabu vya falsafa wa Tanzania Dk. Adolf Mihanjo anasema katika kitabu chake cha ‘Falsafa na Ufunuo Wa Maarifa’ kuwa kuzuia changamoto kutoka kwenye fikara huru kunatufanya tushindwe kugundua ukiini wa mijengeko ya fikara katika nchi mbalimbali za Ulaya na hivyo kuzipokea katika mazingira ya ushabiki wa tumbo na njaa bila fikara sahihi za Kitanzania.

Nimesoma kwa makini sana changamoto alizotoa Padri Privatus Karugendo katika makala yake kwenye RAI toleo NA 693 ya Januari 18 – Januari 24, 2007 yenye kichwa cha habari “REDET ni jukwaa huru”, aliondika kukanusha makala niliyoandika kwenye RAI toleo NA 692 ya Januari 11 – Januari 17, 2007 yenye kichwa cha habari “Wasomi Msitumike Kupotosha Umma”.

Padri Karugendo ameandika makala hii kwa ushabiki-binafsi wa kutaka kutakasa maovu ya REDET kwa kutumia sanaa ya mpangilio wa maneno kuliko uzito wa maudhui wa utetezi wake, kama Padri utakaso wa aina hii ni kukufuru.

Inavyoonekana ni kuwa Padri Privatus Karugendo hakubaliani kuwa wasomi wanaweza kutumika kupotosha umma wa watu.

Na pengine hisia zake katika kuibua dhana hiyo ilikuja pale aliposhiriki kongamano za REDET na kuwaona maprofesa na madaktari waliowasikivu wa hoja na kuongea kwa kujenga hoja.

Hilo ni suala jema kwa wasomi kujenga hoja katika mujukwaa yao wenyewe na wasomi au watu walio na uwezo huo.

Jukwaa huru ya REDET alioiona Padri Karugendo ni kivuli tu ambayo Padri Karugendo haoni kabisa watu halisi waliopo na pengine niseme alikuwa na papara zaidi kukimbia kujibu hoja hii.

Ni nafasi yangu kumweleza huyu ndugu yangu kuwa rushwa za kisomi (Intellectual corruption) ni tatizo kubwa sana duniani kwa sasa, na ni moja ya rushwa mbaya sana kwa maana inawafanya wasomi kutumia nafasi zao za kuaminika katika jamii kupenyeza sumu za tafiti ambazo nyingi lengo lake ni wao na wafadhili wao kunufaika.

Hii ni rushwa mbaya kuliko rushwa ya wanasiasa ambao wao uchukua pesa tu na kutumia kwa shughuli zao na miradi yao.

Ukisoma katika gazeti la The Guardian la tarehe Agosti 7, 2003 Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu Benjamin Mkapa anakemea wasomi na watafiti wanaotumia pesa za wafadhili kutoa matokeo ya tafiti ambazo zinahujumu na kupumbaza akili za watu.

Mkapa ananukuliwa akisema kuwa hakuna rushwa mbaya kama rushwa ya kisomi (Intellectual corruption).

Nanukuu alichokisema Rais Mkapa, “Tuna wasomi na watafiti walionunuliwa na wafadhili, ambao wako tayari kupindisha matokeo ya tafiti zao kuridhisha matakwa ya yule aliyewadhili, inawezekana kuwa mfadhili akawa serikali, mashirika au mtu binafsi kwa matakwa yake.”

Hiyo ni kauli wa aliyekuwa Rais wa nchi Benjamin Mkapa, anayeijua nchi hii kwa mapana kuliko Padri Karugendo, aliyeiongoza nchi hii kwa miaka 10, anakiri kuwa kuna rushwa ya kisomi na anasema kuwa ni mbaya.

Rais Mkapa anasema kuwa ni hatari sana kama hizi tafiti zikitumika katika vyombo vya habari na waandishi wasio wadadisi kwa maana mara tu tafiti hizo zinapotumika huingia katika akili za watu na kuwa sehemu ya mitazamo yao.

Hoja ya Padri Karugendo kuwa REDET inafanya utafiti, ina madakatari na maprofesa wapole wanaosikiliza hoja, haiondoi ukweli kuwa REDET inatumiwa na serikali kueneza propaganda na kumjengea Rais Jakaya Kikwete jina kila mara inapohitajika kufanya hivyo.

Padri Karugendo akiendelea kuona mambo katika mtazamo wa macho na sio mtazamo wa kifikara, atakuwa anajenga hoja kwa kuona vivuli vya mambo bila kuingia katika undani na hivyo ataanza kujengea watu vijimungu vya fikara (idols of mind).

Utetezi wa REDET aliohutumia Padri Karugendo inaonyesha kabisa kuwa anauhusiano wa moja kwa moja na REDET, na akifikiri kuwa REDET ikinialika katika makongamano yake kutanijengea uoga wa kujenga hoja yangu.

Hii ni kasumba mbaya ya kufikiri kuwa ujenzi wa hoja ipo kwa tabaka la watu fulani, elimu na kabila. Na kama ndivyo ndugu yetu Karugendo anavyoishi basi anawaweka miungu wengi mbele ya fikara zake na sio muda mrefu atajikuta akiwa mtumwa wao.

Sipendi kurudia nilichokiandika katika makala yangu iliyojibiwa na Padri Karugendo kwa kuhofia kujaza kurasa nyingi.

Inavyoonekana ni kuwa Padri Karugendo haamini kuwa wasomi na vile tu kuwa maprofesa basi wanasiasa hawawezi kujipenyeza na kuwatumia wanavyotaka.

Padri Karugendo alitegemea kuwa katika warsa aliohudhuria pale chuo kikuu alipoona mjadala huru ilimtosha kuiona REDET katika uhalisia wake.

Nataka nimpe Karugendo dondoo kidogo jinsi asasi nyingi za kisomi zilivyokwishatumika katika nchi mbalimbali duniani kueneza propaganda za kisiasa kwa wananchi.


Kabla ya yote ni vema nimweleze Karugendo kuwa kuna asasi za aina nyingi na chache kati yake ni kama zifuatazo; kuna asasi zisizo za kiserikali (NGO — Non-Governmental Organization), Asasi za kiserikali (GONGO — Governmental NGO), Asasi inayofanya kazi za Kiserikali na isiyo ya Kiserikali (QUANGO — Quasi NGO), Asasi zenye uhusiano na Serikali (GRINGO — NGO with a symbiotic relationship with a government), Asasi za vyama (PANGO — Party-affiliated NGO hizi zipo sana Latin Amerika), Asasi za wafadhili (DONGO — Donor-organized NGO), Asasi za wafanyabiashara (BINGO — Business NGO) na Asasi za kijamii (CSO — Civil Society Organization).


China imekuwa ikitumia sana QUANGOs au GRINGOs ambayo imekuwa ikianzishwa na wadau na mara nyingi wasomi na watu maarufu sana wanaojifanya kuwa watetezi wa wanajamii kumbe kwa chinichini wanatumiwa na serikali kupenyeza kwenye akili za watu mambo ambayo wanajua kabisa watu hawawezi kuzikubali bila kwanza kutumia QUANGOs au GRINGOs katika kueneza propaganda.


Asasi kama hizi kwa China zilianza kipindi kile cha kueneza propaganda za kikomunisti na sera juu ya Taiwan inayotaka kutambuliwa kama taifa huru dhidi ya China.


Kwa Amerika ya Kusini Wasomi wengi walianzisha Asasi za kueneza sera ya vyama vya siasa (PANGO — Party-affiliated NGO) ingawa hawajionyeshi waziwazi na pengine vyama hivi uwapatia watu hata misaada katika mahitaji yao na kisha kukubalika katika vichwa vya jamii hiyo mara moja hutumia nafasi ile ya kuaminika kueneza propaganda.


Na kwa mfano huu REDET ni kama GRINGO na QUANGO kwani hujifanya kuwa huru ili iaminike huku ikitumika chinichini kueneza propaganda za serikali. Na kama huo ndio Jukwaa Huru alioona Karugendo basi inabidi avae miwani yenye lensi.


Gazeti la The Washington Post la Machi 9, 2006 limeandika juu ya viongozi wa chama cha Demokratiki cha Marekani wakiituhumu serikali ya Rais Bush kwa kutumia Asasi nyingi kupita kiasi kueneza propaganda za chama chake huku zikiwa zimejificha kama asasi za kisomi na watu maarufu nchini.
Gazeti la The Economist la Januari 29, 2000 lililochapishwa likiwa na maandishi makubwa “The Sins of NGOs (Dhambi Kubwa Zinavyofanywa na Asasi)” na kwa chini yake iliandikwa kwa maandishi madogo ikiuliza “Are these Governments' puppets? (Je asasi hizi ni vibaraka wa serikali?) ilinukuliwa ikitoa lawama kwa asasi za wasomi wa Ulaya wanaotumia wasomi wa nchi za Kiafrika kufanikisha mambo ambayo pengine hayamstahili hata mwafrika ila mara nyingi inakuwa ni sehemu za sera za nchi za nje.
Kwa mifano hiyo michache itampa Padri Karugendo picha ya ndani ya baadhi ya mambo yanayofanywa na asasi nyingi hapa Tanzania na nje.
Nasema sio kila asasi inatumika, sio kweli, nimeona asasi kama Haki Elimu na mengine mengi ikifanya kazi yake vizuri na unaweza ukanona dhamira ya uzalendo ndani yake.
Lakini asasi hii ya hawa wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) imeanza kuleta wasiwasi juu ya kazi tafiti zake za kisiasa na hasa zile zinazoonyesha kumjenga Rais jina kila mara.
Padri Karugendo ungetegemea mshauri wa Rais kama alivyo Prof. Mukandala angeweza kutumia Asasi ambayo yeye ndiye kiongozi wake kutoa takwimu halisi hata kama zingeonyesha kuwa watu wamemchoka huyo Rais?
Unategemea kuwa REDET ingeweza kuikosoa Serikali ambayo tayari kiongozi wake anaishauri (advisory input), kwani kwa kuiokosa serikali Rais angeweza kumuuliza kuwa kwa nini yeye kama mshauri asingemshauri hilo alilolisema kabla ya kuiibua kwenye majukwaa ambayo Karugendo anayaita huru.
Karugendo anazungumzia mtindo wa kura ya maoni kwamba unatumika hata kule Amerika, lazima ajue kuwa hata kule Amerika asasi zinazoendesha hizi kura ya maoni nyingi ni za vyama, utakuta moja inatoa ripoti kutetea chama cha Republican au kutetea Democratic.
Lazima ijulikane kuwa kura za maoni ya Amerika ni za gharama ndogo kwani wengi hupiga kura hizo kupitia kwenye mitandao ya tovuti na blogu (Online poll) ambazo ni nyingi na hazina gharama ukilinganisha na tafiti za chuo kikuu ambazo lazima ziandaliwe dodoso, wachague kikundi (sample) na hivyo kuna hatari za kuchagua eneo ambalo lina mtazamo mmoja wa kisiasa.

Kwa mfano ukitumia Pemba kutoa maoni juu ya Rais Abeid Karume na Rais Jakaya Kikwete ni wazi kuwa Rais Kikwete ataonekana kuwa watu wengi kutokana na siasa za Zanzibar.
Na ili kuhalalisha matokeo ya kura hizo za maoni zilizochukuliwa katika mikoa mitatu tu au minne ni kuyatangaza kuwa ni maoni ya Watanzania imekuwa mwanya ya kuwepo kwa propaganda.
Karugendo lazima ajue kuwa online poll za Amerika ni nyingi sana kiasi kwamba wananchi wa Amerika wamekuwa wakitilia mashaka kwa maana watu wengi wana blogu zao na tovuti zao.
Hatukatai na vilevile ni makosa kusema kuwa REDET haijafanya lolote la maana, lakini kutumia muda mwingi kulimbikiza umaarufu wa mtu mmoja kwenye vichwa vya wananchi.
Niliandika kuwa REDET wameanzisha chuo huko Zanzibar iitwayo Democracy Training College (DTC) ikiwa na lengo la kuwafundisha vijana wa Zanzibar juu ya ‘Political Tolerance (Uvumilivu wa Kisiasa)’.

Nilisema namna nzuri ya kutatua mgogoro Zanzibar upo kwa viongozi wenyewe, kwa maana duniani sasa hivi siasa inayotumika hata kwa majirani zetu nchini Kenya wameshajua kuwa ni kuunda serikali ya mseto (coalition government) au vyama vya mseto (Alliance parties), lakini leo hii Karume anasema kuwa aliye na hiyo hoja aipeleke Zanzibar, aamini kama hicho kinawezekana.

Kwa maana nyingine huo msemiati wa serikali ya mseto haipo katika kamusi ya Rais karume na hivyo kuwatenga Wapemba kwake ni suala sawa tu.

Ndio maana nasema suala la amani Zanzibar ni suala ya mfumo mbovu wa kisiasa na sio elimu ya Uraia.

Kwani Karugendo anataka tuamini kuwa Tanzania Bara iliyo na amani, watu wake wana elimu kubwa ya uraia na uvumilivu wa kisiasa kuliko watu wa kisiwa cha Zanzibari iliyo na mgawanyiko wa kisiasa?

Mbona REDET inamkwepa mtu muhimu (Rais karume) ambaye akipata elimu hii basi Wapemba na Waunguja watakuwa na mfumo linganifu wa kisiasa.

Karugendo anatetea na anataka tuamini kuwa kwa kuwapa vijana wa Zanzibar elimu ya uvumilivu wa kisiasa hata kama kukiwepo na mfumo dume wa kisiasa visiwani kuwa hiyo italeta amani.

Hizi ni fikra ni potofu, ni za kukwepa majukumu, na ni sawa na hadithi za panya za nani amfunge paka kengele shingoni.

Pale Wapemba wanapotaka uchaguzi huru na uhesabuji wa kura usioghubikwa na wizi, na kutaka kujiona wao ni wamoja, basi suluhisho waliyoiona REDET ni kuwaanzishia shule ya mafunzo ya Kidemokrasia Democracy Training College (DTC ikiwa na lengo la kuwafundisha vijana wa Zanzibar juu ya ‘Political Tolerance (Uvumilivu wa Kisiasa)’.

Sijui kama ndugu yangu Karugendo naye ana wasiwasi kuwa kwa mbinu hizi za kilaghai REDET kama wameanzisha chuo cha uvumilivu wa kisiasa (political tolerance) sio muda mrefu itaanzisha chuo cha Uvumilivu wa Rushwa (Corruption tolerance).

Na ndio maana naamini kauli za James Reeves aliyoiandika katika kitabu chake cha “The Confusion of the Scholars (Mkanganyiko kwa Wasomi) kuwa baada ya siasa kuonekana inalipa kuliko tafiti na uhadhiri wasomi wetu wameamua kujibwaga katika siasa bila kuangalia, kurekebisha, kutetea na kujali hata athari za mfumo hiyo mibovu wanayoihunga.

Lakini kinyume chake wasomi wetu wamekuwa wakitumia mapungufu ya kijamii kujineemesha, kama vile demokrasia, haki za binadamu, haki za wanawake na mgawanyiko wa kisiasa kuhujumu fikra za waafrika na mwelekeo mzima wa maisha ya mwafrika, na hao ndio Padri Karugendo anawatetea.


0715 551455
http://nyasigo.blogspot.com

2 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...
This comment has been removed by the author.
kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...
This comment has been removed by the author.