Saturday, January 13, 2007

Waalimu wa Sita


Waalimu wa Sita wasiwambwe msalabani

Na Nyasigo Kornel

Mshairi maarufu sana wa Uingereza aitwaye Shakespeare, katika tungo za mashairi yake aliwahi kuandika kuwa‘One way to get an education in a hurry is to drive a school bus’ (Njia mojawapo ya kupata elimu kwa haraka zaidi ni kuendesha basi la shule).

Hii ina maana kuwa kadri unavyokuwa karibu na watu wenye maarifa na ujuzi wowote basi uwezekano mkubwa wa kupata huo ujuzi kwa haraka ni mkubwa.

Siku sio nyingi waalimu waliopata mafunzo ya mwezi mmoja mara baada ya kuhitimu kidato cha sita wakijulikana kama ‘Waalimu wa Sita’ walikuwa wakipata changamoto katika vyombo vya Habari kuwa hawawezi kumudu kufanya kazi katika taaluma hiyo kwa muda huo mfupi wa mafunzo.

Imefikia hatua waalimu na wanafunzi katika mashule yao wanayofundisha wanawanyanyapaa na kuwapa majina mabaya sana kitaaluma wakiitwa ‘mabambucha’.

Wanasema nyani huchekana ngoko, hoja ni kwamba hawa waalimu hawana tofauti kubwa sana na wale waliopo kwani hata wale waliopo hawajathibisha utofauti wao kitaaluma.

Hiki kitendo tu inaonyesha kuwa walimu bado hawajui kuwa China walipokuwa na upungufu mkubwa wa waalimu katika miaka ya nyuma na idadi ya watu ilipoongezeka kuliko idadi ya waalimu, wanafunzi waliachishwa masomo ya sekondari bila mafunzo, na kisha waalimu wenzao waliwapa mafunzo wakiwa wanafundisha kwa vitendo.

Mwandishi maarufu wa makala ya elimu Hun Hwang wa shirika la Habari la China liitwalo Xinhua aliandika kuwa waalimu kama hawa walifanikiwa kuleta mapinduzi makubwa ya elimu katika historia ya China. Sababu ilikuwa ni kwamba walitaka kuthibitisha kuwa wao sio wa kiwango cha chini kama ilivyofikiriwa.

Hata katika miaka ya 1980, Indonesia ilitaka kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo na teknolojia, lakini waalimu waliokuwepo hawakuwa wamepata mafunzo sanifu katika nyanja hizi ambazo hapo awali hawakuwa wameipa kipaumbele. Walichoamua ni kuachisha masomo wanafunzi kutoka katika vyuo vya kilimo na ufundi kwenda mashuleni kufundisha.

Hadi hii leo, Indonesia inajivunia mapinduzi makubwa yaliyoletwa na vijana hawa na ni hapo ndipo hata wanafunzi wa shule za sekondari walipoweza hata kutoa mswada katika viwanda juu ya namna ya kutengeza pembejeo ya aina Fulani.

Utaratibu huu uitwa ‘crush program’ na inatumika pale ambapo serikali imeshindwa kuwianisha mipango ya muda mrefu na mahitaji ya jamii kama ongezeko la watu, hivyo inaamua kuzima moto kwa njia hii.

Badala ya kuzomea waalimu wazoefu kuwazomea waalimu hawa wa Sita wanatakiwa wawasaidie, huu ni upungufu mkubwa wa saikolojia ya mahusiano ambayo waalimu hawa ndio wataalamu wa masomo hayo.

Ukisoma katika kitabu cha ‘pedagogy of the Oppressed’ kilichoandikwa na msomi maarufu wa Brazil bwana Paulo Freire ambaye ameshiriki katika mapinduzi makubwa sana ya elimu nchini hapo, kinasema kuwa ‘teachers are not trained in the classroom but in the fields’ (waalimu hawaandaliwi madarasani bali wakiwa mazoezini).

Katika kitabu cha Prof. Ronald Dore kiitwacho ‘Diploma Disease’ (Magonjwa yatokanayo na kupata Stashahada) aliandika juu waalimu waliokuwa wakifikiri kuwa vyeti vyao vya diploma vingeweza kufanya kazi yenyewe mara baada ya kuhitimu bila jitihada za mwalimu kuwa mbunifu.

Prof Dore anasema kuwa siku hizi kazi ya ualimu unapatikana kwa maonyesho ya vyeti vya diploma na shahada. Anasema kuwa mashule yetu yamejaza waalimu wenye vyeti hivi vya diploma na shahada ambao wengine hawawezi hata kuongea mbele ya wanafunzi na wala sio hata wabunifu.

Aliuona ugonjwa huu wa diploma uliokuwa unawasumbua waalimu katika nchi nyingi alizofanya utafiti wake ikiwemo nchi ya jirani ya Kenya, Japani, Sri Lanka na Uingereza.

Huu ugonjwa wa diploma upo hata hapa Tanzania, tena umefanya hata hii taaluma ya ualimu kudharaulika. Na wanaofanya ualimu kuonekana kama ni taaluma ambayo kila mtu anaiweza ni hao hao waalimu wenyewe.

Miezi miwili iliyopita nilishiriki katika Warsha ya wiki moja iliyokutanisha baadhi ya waalimu wenye uzoefu wa kufundisha sayansi katika nchi za maziwa makuu mjini Nairobi, Kenya.

Ingawa nilishiriki kama mwandishi lakini mafunzo yangu ya ukufunzi wa masomo ya sayansi kwa vyuo vya ualimu ilinipa nafasi ya kujionea fikira potofu ambayo kama waalimu hawatayafuta basi hatutang’oka.

Moja ya mada iliyojadiliwa na waalimu hao wazoefu ilikuwa ni juu ya vikwazo wanazopata katika kufundisha masomo hayo ya sayansi mashuleni.

Mwalimu mmoja aliyewakilisha Tanzania akitokea Moshi alijibu kwa kusema kuwa hawana vitabu vya sayansi na zaidi aliendelea kuongea kwa jazba akisema kuwa tangu aanze kufundisha hajawi kuona aina yoyote ya kemikali na hata kifaa cha maabara, na zaidi ya yote mishahara ni midogo.

Waalimu wenzake kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walimpigia makofi huku wakiongezea kwa kusema, “sema yote mzee”.

Mwalimu wa kitanzania, tena aliyebora na aliyewakilisha wenzake anasema hajawahi kuona kemikali katika maabara! Je mchanga ni nini kama sio kemikali? Hajui kuwa ‘Calcium silicate’ ndio asilimia kubwa ya mchanga! Je maji ya limau na matunda hajui kuwa ni kemikali?

Mpaka serikali itumie mabilioni ya pesa kuagiza starch ambayo hata mwalimu angetumia ubunifu kidogo akaipata katika unga wa mihogo, sasa hivi starch inaagizwa kwa wingi hadi vyuo vikuu hawatengenezi starch vyao.

Dunia tuliyomo ni Kemikali, fizikia au baiolojia. Ukichukua pombe ya gongo ni kemikali, maji ni kemikali, nyongo ni kemikali, sabuni, maji ya miti, mate, mafuta, matope na mengine mengi.

Kumfundisha mtoto ili aelewe juu ya hewa ya oksijeni na kabondioksidi itakuhitaji kiberiti, mshumaa na mfuniko mkubwa tu kumthibitishia mwanafunzi kuwa kama hakuna hewa ya oksijeni basi mshumaa hauwaki, basi.

Huyu mwalimu aliyepigiwa makofi na walimu bora wenzake wa sayansi, hajawahi kuona kemikali, na hata hana wazo ya kutengeneza maabara ya sayansi inayojumuisha vitu vilivyopo katika mazingira yake. Lakini bado alipendekezwa na lile shirika kuwa ni mwalimu bora.

Na hili ni tatizo lililopo hata kwa waalimu wa chuo kikuu wanaowaandaa hawa waalimu. Leo hii mwalimu wa sayansi anaamini kuwa hawezi kufanya majaribio mpaka starch itoke China na Ufaransa. Hajui kuwa mihogo ni starch.

Leo hii katika Tanzania hii iliyojaa kompyuta na fotokopi karibia katika kila Mkoa wa Tanzania, mwalimu bado darasa lake linakoswa vitabu. Pale panapotokea upungufu wa vitabu vya rejea mwalimu wa kitanzania bado hawezi kutunga hata kitini na akapiga fotokopi kuziba pengo la vitabu.

Mwalimu wa darasa la kwanza anasubiri aletewe vitabu vya kujumlisha vilivyochapishwa na ‘Mture Book Publishers, Macmillan Aidan, E&D Publishers na Oxford University Press’. Aletewe vitabu vyenye silabi ‘a, e, i, o, u’ na vile vya namna ya kuandika mchorongo. Kwani mwalimu hawezi kutunga kitabu kimoja wakapiga fotokopi ikatosha darasa zima.

Mwalimu wa kitanzania hawezi kutunga hata kitabu ili kitumike shuleni, hata ya kujumlisha, za silabi, za kusoma na kuandika. Alafu leo waseme wanalo la kujivunia juu ya waalimu wa Sita! Wote wanafanana na kama utofauti upo ni mdogo sana unaoweza kuzibika kwa muda mfupi sana.

Ni waalimu wangapi wamejadiliana na Afisa Elimu wa Wilaya juu ya hilo wazo mbadala, na badala ya pesa za MMEM na MMES kununua vitabu vya makampuni makubwa waalimu wa aina hii wapewe ruzuku kama kazi zao ni nzuri.

Siku ya mwalimu duniani, mwalimu mmoja aliye na shahada ya sayansi aliongea katika runinga akisema kuwa shule yake aina hata kitabu kimoja cha fizikia. Mimi nafikiri huu ndio uvivu, uzembe na ujinga. Mtu wa chuo kikuu hauwezi kupambana na mazingira yako, na kutoa utatuzi wa tatizo hilo dogo.

Hivi kweli watoto wetu wasisome kwa kukoswa vitabu na mwalimu wa hilo somo ana shahada! Kama sio ugonjwa wa shahada au ugonjwa wa diploma ni nini sasa? Je mwalimu wa hivyo ni urithi kwa nchi hii kweli?

Wakati mwingine tumekuwa tukiilaumu serikali bure. Kama mtu amelipiwa na hiyo serikali yake na kusoma ili aisaidie nchi yake anakaa katika shule ambayo haina hata kitabu wala maabara, na anashindwa kuorodhesha aina ya mimea kisha akawahusisha wanafunzi wake, wakakusanya jamii mbalimbali ya mimea yenye misingi ya kisayansi na kisha wakatengeneza bustani ya botania.

Leo hii huyu mwalimu wa aina hii naye eti anamcheka mwalimu yule wa Sita kuwa hawajapata mafunzo ya kutosha. Mnawazidi nini?

Kuna lugha inayotumika katika ualimu inayoitwa ‘tabula rasa’ ikiwa na maana kuwa chombo tupu. Na mwalimu anashauriwa asimfanye mwanafunzi ‘tabula rasa’ kwa kumtafunia kila kitu na mwanafunzi kumeza tu.

Sasa hivi inavyoonekana ni kuwa waalimu ndio wamekuwa ‘tabula rasa’ na sio wanafunzi tena.

Plato mwanafalsafa aliyetoa nadharia nyingi sana katika elimu ay ualimu anaamini kuwa mitaala ya elimu ni vichocheo tu vya kuamsha elimu na maarifa na siyo viletavyo maarifa, hivyo anasisitiza majadiliano kama njia ya kuamsha maarifa nadni ya mwanafunzi.

Lakini mwanafalsafa mwenzake kama Aristotle anapingana naye kwa kuamini kuwa binadamu hazaliwi na maarifa bali huzaliwa na uweza wa kujua na kadri anavyokumbana na vitu vinavyoonekana ndivyo anavyopata maarifa.

Duche Smith aliwahi kuanzisha shule ya ualimu nchini Uingereza katika mtindo wa wanafalsafa hawa wawili yaani Plato na Aristotle, ambayo waalimu waliofuzu katika chuo chake walikuwa wakitafutwa kama keki duniani. Wale waalimu wa Duche hawakuhitaji hata vitabu na maabara. Wao walitaka wapewe mitaala tu. Walikuwa na msemo uliowasifia mbinu zao ikisema ‘just curriculum will show the means and ends’ (mitaala itaonyesha njia na matokeo yanayokusudiwa).

Hawakuwa waalimu wanaoogopa wakaguzi, hawakusimamiwa, walikuwa wakijiamini na kufanya kazi zao kwa hali ya juu sana. Walisaidiana na wanafunzi wao kuandaa vifaa vya kujifunzia hata notisi za mwalimu mwanafunzi aliweza kumletea hiki na kile akaongezea.

Dhana ya mwalimu kuibulia wanafunzi fikara pevu na kuwa na jamii ya watu wanaoweza kusimama na kudai haki zao hata pale wanapoonewa imekwisha potea.

Waalimu wamekuwa wakisubiri kusemewa hata katika mambo yanayohusu taaluma yao.
Huliza wakwambie kama hata wanapobadilisha mitaala kama wanashirikishwa!

Siku chache kabla ya ule mtaala wa Waziri wa awamu ya Tatu wa Wizara ya Elimu na Utamaduni Joseph Mungai kukataliwa, ni waalimu wasiofika 100 tu ndio waliokutana, na si ajabu hao waalimu waliokutana hawakuwa na uwezo yakinifu juu ya uchambuzi wa mitaala.

Sasa hivi utaona vitabu ambavyo wanafunzi wasoma, ni vile vitabu ambavyo haviibuhi fikira pevu kwa kizazi hiki tulichonacho. Ingawaje hatuna vile vitabu vingi vyenye kuibua ukombozi wa kifikra, lakini ijulikane kuwa wanasiasa wanataka watu wasifumbuke akili, wanataka tuwe madondocha ili wao na watoto wao watutawale bila kuzinduka.

Mwalimu Nyerere alichekesha akisema wanasiasa wanasema ujinga ni baraka.

Tazama, katika vitabu vya fasihi kwa shule za sekondari mwanafunzi anapewa kusoma kitabu kama ‘penzi kitovu cha uzembe au kile cha Hiba ya Wivu’ nyingi ni vitabu vyenye ladha ya mapenzi, na wanajua kuwa wanafunzi wetu wanapenda mambo ya mapenzi mapenzi, lakini ni nani aseme? Waalimu wako kimya, wanavichukua na kisha kuingia darasani na kuanza kuwacheulia watoto wetu.

Vitabu vyenye silika za ukombozi hawawezi kamwe kuwapatia wanafunzi wetu kama Almasi za Bandia kilichoandikwa na marehemu Prof. Seith Chachage, Makuadi wa soko huria na mengine kama hayo.

Mwanafunzi wa sekondari aliyesoma vitabu vya fasihi laini laini hizi za mapenzi huwezi kumlinganisha na yule anayesoma fasihi zenye falsafa na hamasa nzito kama vilivyoandikwa na mrusi Marxim Gorky ‘mama’ mrusi aliyetetea wafanyakazi wa viwandani hata kuleta mapinduzi ya viwanda.

Gazeti la NewYork Times liliandika kwa mandishi makuwa kabisa kuwa ‘teaching children to count is not as important as teaching them what counts’ (kumfundisha mtoto kuhesabu sio muhimu kama kumfundisha kuelewa yaliyobora.

Watu wengi walioshiriki katika ukombozi wa dunia hii waliibua vichocheo hizo wakiwa bado wapo mashuleni. Angalia historia ya Pan-African na hata maandamano yaliyofanywa na wanafunzi wa Soweto huku Afrika ya Kusini.

Mwalimu wa kitanzania hawezi kusema, hawezi kuuliza juu ya mtaala anaoletewa autumie, haulizi hata juu ya vitabu anavyotakiwa mwanafunzi aisome.

Ivan Illich, katika kitabu chake maarufu sana kwa wasomi wa elimu kiitwacho Celebration of Awareness, anawabeza waalimu ambao wakishapata vyeti wanalala, wanasherehekea kiwango chao cha uelewa, shahada zao na diploma hizo, hawajishughulishi kuibua mapinduzi ya kifikira katika taasisi za miongozo yao.

Ukitaka kujua ni kwa kiwango gani haya yametuletea madhara nenda mashuleni, utawakuta wanafunzi wa sekondari wamebeba majarida yale yenye michoro ya michafu kwenye jalada (Sexual arousal magazines). Huyu mwanafunzi, katika umri wa miaka ya sekondari tuseme 20, hataweza kuhoji mambo ya msingi yanayohitaji fikira nzito na huwezi kumlinganisha na mwanafunzi anayesoma vitabu vizuri.

Haitoshi tu kusema kuwa mwalimu ana diploma, shahada au amepata mafundisho ya mwezi mmoja. Tunataka tuwaone kwa matunda yao.

Hata yesu aliwaambia kuwa siku yaja ambapo kutakuwepo na manabii wengi hata wa uongo lakini alipoulizwa kuwa watawajuaje, aliwajibu wanafunzi wake kuwa mtawajua kwa matunda yao.

Simu: 0715 551455
Email: emmakornel@yahoo.com


No comments: